Kauli za ‘kisiasa’ zinavyovuruga elimu ya Tanzania

Kauli za ‘kisiasa’ zinavyovuruga elimu ya Tanzania

Mastaajabu hayajapoa katika sekta ya elimu nchini. Ukisahau walimu wa UPE miaka ile ya 1970 au wale wa ‘Voda Fasta miaka ya 2000’, utakutana na uamuzi wa kufuta masomo ya kilimo na michezo.

Hii ndiyo sekta ya elimu ambayo kwa miaka nenda rudi, baadhi ya maamuzi yanayofanywa na watendaji yamekuwa yakiwaacha midomo wazi Watanzania.

Kibaya zaidi ni maamuzi yanayoacha athari hasi katika sekta ya elimu. Fikiria kwa mfano, mwanafunzi wa shule ya msingi anayefundishwa na mhitimu wa elimu ya msingi!

Au Taifa limeathirika kwa kiwango gani kufuatia uamuzi wa masomo ya michezo na kilimo kufutwa wakati wa utawala wa Serikali ya awamu ya tatu?

Wakati kumbukumbu hiyo ikiwa haijapoa kwenye vichwa vya Watanzania, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, hivi karibuni ilisitisha utekelezaji wa mtalaa mpya wa kidato cha tano.

Uamuzi huo umekuja wakati tayari wanafunzi walisharipoti shuleni. Baadhi sasa watalazimika kubadili tahasusi ili kwenda sambamba na mahitaji ya mtalaa wa zamani unaoendelea kutumika.

Akifafanua sababu ya kurudi kutumia mtalaa wa zamani badala ya mpya, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkanda alisema kuna sababu za kiufundi zilizochangia kuahirishwa kwa utekelezaji wa mtalaa huo kwa wanafunzi wa kidato cha tano.

“Mojawapo ya sababu za kiufundi, ni printing (uchapishaji) ya vitabu haijakamilika na bahati mbaya printing ya vitabu haifanyiki nchini lakini ni jambo ambalo tutakuja kulibadilisha,”alisema hivi karibuni akiwa jijini Dodoma.

Alisema walikaa na wadau na kwa pamoja walikubaliana kuahirisha mtalaa huo kwa sababu yaa uwezekano wa kuchelewa kusambaza kwa vitabu shuleni.

Profesa Mkenda alisema kuwa baadhi ya wanafunzi wameelekezwa kubadilisha tahasusi walizochagua.

Mbali ya hilo, makala haya yanaangazia baadhi ya maagizo kwenye sekta hiyo yaliyowahi kuibua mjadala mzito

Walimu wa UPE

Elimu kwa Wote ambayo ni tafsiri ya maneno ya Kiingereza Universal Primary Education (UPE), ulikuwa mkakati muhimu wa Serikai miaka ya 1970, ukilenga kuchochea kasi ya maendeleo ya nchi kupitia kufuta ujinga, umasikini na maradhi kwa nchi ambayo miaka michache nyuma ilikuwa imetoka kupata uhuru.

Ili kurahisisha upatikanaji wa elimu kwa kila mtoto wa Kitanzania pasipo ubaguzi, Serikali ilichagua wanafunzi waliohitimu darasa la saba, ikawanoa kwa minajili ya kwenda kufundisha wanafunzi wa elimu ya msingi.

Kifupi mhitimu wa elimu ya msingi alifunzwa kuwa mwalimu wa wanafunzi wa elimu ya msingi!

Kufutwa kwa masomo ya kilimo

Aliyekuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni katika Serikali ya awamu ya tatu, Joseph Mungai, alifuta masomo ya kilimo.

 Si kilimo pekee, waziri huyo pia alifuta michezo akidai kuwa iliwakosesha walimu na wanafunzi muda wa kufundisha na kujifunza.

Kuchanganywa masomo ya sayansi

Kioja kingine kilichofanywa uongozi wa Mungai ulikuwa agizo lake la kuchanganywa kwa masomo ya kemia na fizikia na kuwa somo moja, kwa hoja kuwa silabasi ya sekondari ilikuwa na masomo mengi hali iliyochangia ugumu wa ufundishaji wa masomo ya sayansi, lugha na Hisabati.

‘’Tulijitahidi kupunguza wingi wa masomo na kuongeza vipindi vya lugha na hisabati viwe kila siku… Kitaaluma unaweza kusoma somo la sayansi ndani yake zikiwamo mada za biolojia, kemia na fizikia…’’ alijitetea Mungai alipohojiwa na gazeti hili Machi 16, 2013.

Walimu wa Voda Fasta

Baada ya hamasa kubwa ya uongozi wa awamu ya nne kutaka kujengwa kwa shule za sekondari kwa kila kata, shule hizo zilijikuta hazina walimu.

Kutatua tatizo hilo, Serikali iliwashangaza wadau wa elimu na wapenda maendeleo nchini kwa kuruhusu utolewaji wa mafunzo ya muda mfupi kwa walimu. Walimu hawa waliomaliza kidato cha sita maarufu kwa jina la utani la Voda fasta walifundishwa kwa muda wa wiki sita na kisha kupewa leseni ya kufundisha. Kwa kawaida walimu wa cheti na diploma husomea miaka miwili na wa shahada kati ya miaka mitatu na minne.

Kufutwa makali mtihani wa kidato cha pili

Mwaka 2008, Serikali ilipunguza makali ya mtihani wa mchujo kwa wanafunzi wa darasa la nne na wa kidato cha pili iliposema “mitihani ya ngazi hiyo isiwe kikwazo cha maendeleo ya elimu.”

Kauli hiyo ya aliyekuwa Rais, Jakaya Kikwete ilichukuliwa kama agizo kwamba wanafunzi waliofeli waruhusiwe kuendelea na masomo ya darasa la tano hadi la saba na kidato cha tatu hadi cha nne.

Moja ya athari za kufutwa kwa mitihani hii ni kuwajengea au kuhamasisha uvivu wa kujifunza miongoni wa wanafunzi, kwani walibweteka wakiamini kuwa hakukuwa na kikwazo cha kuwazuia kufanya mtihani wa darasa la saba na wa kidato cha nne.

Mbumbumbu wachaguliwa sekondari mwaka

Kama kuna vioja ambayo havitosahaulika katika historia ya nchi hii ni pamoja na kuwapo kwa taarifa za wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza.

Aprili 2012, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ilibaini wanafunzi 5,200 waliojiunga sekondari walikuwa hawajui kusoma wala kuandika. Swali kuu lilikuwa walifaulu vipi?

Kuua daraja sifuri, kuanzisha daraja la tano

Serikali ya awamu ya nne iliwahi kutoa uamuzi uliowaacha watu wengi midomo wazi. Huo ni uamuzi wa kupunguza alama za ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne, huku ikiua daraja sifuri na kubuni kile Serikali ilichokiita daraja la tano. Baada ya wananchi kulalamikia ikaja na mfumo wa ukokotoaji kwa kutumia GPA.

Maoni ya wadau

Mshauri mwelekezi wa Shirika la HakiElimu, Dk Wilberforce Meena anasema mabadiliko ya mara kwa mara katika elimu yanahatarisha mfumo wa elimu nchini.

Anatoa mfano mwaka 2015, Serikali ilianzisha mafunzo ya astashahada kwa ajili ya walimu wa shule za msingi, halafu baadaye mafunzo hayo yakafutwa.

“Mafunzo hayo yalikuja yakarejeshwa tena na kuna wanafunzi walikwenda kujiunga na hayo mafunzo ya astashahada ya elimu ya awali, elimu ya msingi na elimu maalum na wakiwa chuoni Serikali ikafuta,” anasema.

Kwa mtazamo wake, anasema Taifa haliko makini katika kuleta mabadiliko katika mfumo wa elimu.

“Mabadiliko mengi tunayofanya yanaendeshwa na utashi wa kisiasa kuliko misingi ya kisayansi katika kuleta mabadiliko ya elimu,” anasema.

Anasema matokeo yake kama Taifa hatutakuwa na mfumo imara wa elimu utakaotupatia matokeo tunayotarajia katika elimu, na hivyo tutakuwa tunaanza upya hakutakuwa na mwendelezo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet), Ochola Wayoga anasema ni hatari kwa nchi kufanya majaribio ya elimu kwani wanaharibu nguvu kazi ya Taifa.

“Elimu ni bidhaa ya umma na huwa zinalinganishwa; kwa mfano utaona vyuo vikuu vinavyolinganishwa, vyuo vikuu vitatu bora, vyuo vikuu 10 bora, 100 bora.

“Sasa ukiona utekelezaji wa sera na mikakati katika elimu unakuwa wa kuyumbayumba, ujue unadhoofisha nguvu kazi ya nchi.

“Pia elimu yetu inaweza isikubalike kwingineko. Najua wanasiasa wanaweza kukataa hasa hawa waliopo kwenye ngazi za kufanya uamuzi watakwambia Watanzania wanafanya kazi nchi nyingi na wanatoka na elimu hiyo hiyo, lakini elimu bora pia inategemea na uimara wa elimu yenyewe. Huwezi ukawa unafanya majaribio kila siku,” anasema.

Kuhusu uamuzi wa kusitishwa kwa mtalaa wa kidato cha tano, Wayoga anasema:“Ukiangalia sababu zilizotolewa kwenye barua ya kusitisha mitalaa ya kidato cha tano ni kwamba, walimu hawajaandaliwa vya kutosha, vitabu havipo vya kutosha, kwa hiyo tukisema kwamba kidato cha tano wanaoanza sasa wakienda na mtaala huo, kuna watakaopata vitabu na wengine hawatapata,” anasema.

Anaongeza: “Inasikitisha sana, wanafunzi wa kidato cha tano hawafiki 200,000 na kila kitabu ni Sh5,000 zinahitajika nakala ngapi hapo? Huwezi kusema bado hujatengeneza vitabu mpaka sasa. Maana yake ni kwamba sio kipaumbele hicho.”

Aidha, anatoa mfano wa mtalaa wa darasa la tatu, akisema watoto walikwenda shuleni bila kuwa na vitabu. “Sasa hii inayumbisha uimara wa elimu na inaweza isitengeneze wanafunzi wanaotakiwa,’’ anaeleza.

Kwa upande wake, mdau wa elimu, Godfrey Telli akizungumzia hatua ya mtaalaa huo kusitishwa, ameipongeza Serikali akisema imejipa muda wa kutafakari kwa kuwa suala hilo ni zito.

“Hivi vitu vinatakiwa tafakuri, kukaa chini na kuhakikisha kuwa vimekamilika kila mahali na kuhakikisha kwamba vimekamilika kila mahali kwamba hili jambo limekamilika ndipo litekelezwe.

“Hilo la mitalaa nalo wangekurupuka, kwa hiyo kurudi kwao nyuma nawaunga mkono kwa sababu wanazidi kukaa chini na kutafakari ili wasijekwenda mbele halafu wakajikuta jambo halitekelezeki wakaliacha tukarudi nyuma,” anasema.

Anasema mitalaa ni jambo kubwa ambalo majaribio yanatakiwa kufanyika kabla ya utekelezaji.

“Mambo kama haya ya kujaribu jambo halafu unagundua kwamba umekosea, yanatokea kila mahali. Sera ndivyo zilivyo, unaingia halafu unagundua kuna changamoto. Mimi nawasifu Wizara ya Elimu kwa sababu, wamenyenyekea wakarudi nyuma ili watafakari zaidi,” amesema.

Hata hivyo anashauri kuwapo kwa timu ya kufuatilia na kufanya tathmini ili kushauri mambo ya kubadilisha.

‘’ Kuwe na tathmini inayofanywa katika maeneo madogo kama wilaya au mikoa na kisha itekelezwe nchi nzima,’’ anasema.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories

Popular
Chief Editor

Insecurity prompts Zanzibar to review its lucrative island leasing

The Tanzanian central government is planning to boost its security presence in the Zanzibar archipelago. A commission tasked with auditing the country’s security forces was appointed in July by President Samia Suluhu Hassan. It says it is concerned about the situation in the country’s Indian Ocean islands that are under the control of the semi-autonomous Zanzibar local government.Continue Reading