Dar es Salaam. Sakata la kuzuiwa mikutano ya hadhara na ile ya ndani ya vyama vya siasa limechukua sura mpya, baada ya Jeshi la Polisi Tanzania kukanusha zuio la Polisi Wilaya ya Mbagala, Mkoa wa Dar es Salaam.
Kanusho hilo la Polisi Makao Makuu linatokana na taarifa ya Polisi Mbagala kwenda kwa chama cha ACT-Wazalendo kuzuia kufanyika kwa mkutano wa hadhara waliopanga kufanyika leo Jumatatu, Agosti 12, 2024 katika Kata ya Charambe, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam.
Barua ya Polisi Wilaya ya Mbagala kwenda kwa ACT-Wazalendo ya leo Jumatatu, pamoja na mambo mengine imesema: “…napenda kukujulisha kuwa mikutano yote ya hadhara na ya ndani imezuiliwa hadi hapo yatakapotolewa maelekezo mengine.”
Baada ya barua hiyo mijadala imeshika kasi mitandaoni, huku wadau wa kisiasa wakikumbusha kile kilichotokea mwaka 2016 kwa mikutano ya hadhara kupigwa marufuku na kuruhusiwa ile ya ndani.
Zuio hilo la mikutano liliwekwa wakati wa utawala wa awamu ya tano, baada ya utawala wa awamu ya sita kuingia madarakani ukiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan uliliondoa na mikutano kurejea.
Mwananchi lilizungumza na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kutaka kujua undani wa zuio hilo la Polisi Mbagala ambapo amesema kinachojitokeza ni hali ya jeshi hilo kujichanganya, hakuna tamko rasmi lilotolewa la kufuta mikutano ya hadhara na ile ya ndani.
“Kilichotokea naona kama Polisi wamejichanganya, hakuna tamko rasmi lilotolewa la kuzuia mikutano ya hadhara na ya ndani kwa kuwa Jeshi la Polisi lina ngazi aulizwe msemaji wake anaweza kuwa na majibu sahihi,” amesema Jaji Mutungi.
Katikati ya mijadala hiyo, saa 8:20 mchana, Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime akatoa taarifa kwa umma akisema: “Jeshi la Polisi lingependa kutoa taarifa kuwa halijapiga marufuku kufanyika mikutano ya nje ya hadhara na ile ya ndani, ili mradi inafuata matakwa ya sheria za nchi.”
“Kilichopigwa marufuku ni mkusanyiko uliokuwa umeitishwa na viongozi wa Chadema huko jijini Mbeya, kwa kivuli cha kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani,”ilieleza taarifa hiyo.
Source: mwananchi.co.tz