Huduma Zimezorota Hospitali Ya Rufaa Mnazi Mmoja Zanzibar

Huduma Zimezorota Hospitali Ya Rufaa Mnazi Mmoja Zanzibar

HUDUMA ZIMEZOROTA HOSPITALI YA RUFAA MNAZI MMOJA ZANZIBAR

Huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Zanzibar zimezidi kuzorota huku wananchi wengi wakilalamikia uongozi wa Hospitali hiyo na watendaji wake.

Wananchi mbalimbali wanaofika katika Hospitali hiyo wanalalamikia kuzorota kwa huduma na kutolewa kwa huduma duni kwa baadhi ya mahitaji pamoja na wagonjwa na wanaokuja ama kutazama wagonjwa au kuwaleta wanatolewa lugha isiyo ya kiungwana.

“Uzembe umekuwa mkubwa katika Hospitali hii, dawa nyingi hakuna, hapa kilichokuepo ni kumuona daktari tu na huyu daktari wakati mwengine humuoni unaambiwa hayupo au kamfuate sehemu fulani na teksi” Alilalamika mmoja wa wananchi aliyempeleka Baba ake mzazi kutibiwa.

Habari zaidi zinaeleza kuwa kumekuwa na tatizo la upatikanaji wa dawa wagonjwa wanaelekezwa wakanunue katika maduka ya kuuza dawa yaliyopo nje ya Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja.

Mama mmoja aliyempeleka mwanae kujifungua akitokea Hospitali ya Makunduchi Mkoa Kusini Unguja alikumbana na kauli mbaya na uzembe kutoka kwa wafanyakazi huku akisubiri kwa saa kadhaa kumuona daktari licha ya kupelekwa hapo akitokea Makunduchi.

Huduma za Lifti katika Hospitali hiyo nazo si za kuridhisha, mara kwa mara wananchi wamelamika kutumia ngazi badala ya Lifti zinakwama na inachukua muda kuzikwamua.

Taarifa zaidi kutoka kwa wagonjwa waliolazwa katika Hospitali hiyo zinasema kwamba wodi wanakolazwa Watoto wenye matatizo mbalimbali, wodi ya watu wazima wanaume na wanawake hazina wavu wa kuzuia mbu.

“Hali ndio kama hivi unavyojionea mwenyewe, saizi ni Magharibi madirisha hayafungi, hakuna wavu wa kuzuia mbu na hapa pana mbu wengi sana unaletwa kwa maradhi mengine unakuja kupata Malaria hapa Hospitali” Alilalamika Mgonjwa Mmoja katika Wodi walioumia miguu.

Aidha, huduma za vyoo katika Hospitali hiyo ni mbaya, hakuna usafi unaozingatiwa wahudumu hawasafishi kwa wakati na inavyostahiki zaidi ya kuondosha njiani.

Baadhi ya huduma katika Hospitali hiyo lazima ue na uenyeji bila ya hivyo itakuchukua muda na hata siku kadhaa kuweza kupata. Mmoja wa wafanyakazi ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema wanakabiliwa na changamoto nyingi huku akilaumu uongozi wa Hospitali hiyo kutosikiliza maoni yao wafanyakazi.

kwa muda mrefu sasa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja imekuwa
ikilalamikiwa na watu wengi sana kutokana na huduma ambazo zinatolewa na wahudumu wake baadhi yao, kuwa wanawatolea maneno na kauli mbaya kwa wagonjwa.

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year’s Most Read News Stories