
Dodoma.Tanzania imekuwa ni miongoni mwa nchi ambazo bado zinakabiliwa na changamoto ya udumavu wa kimo na akili kwa watoto.
Changamoto hiyo imebainishwa kwenye ripoti ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania wa mwaka 2022, kwamba mtoto mmoja kati ya watatu wenye umri kati ya mwaka 0-5 wanakabiliwa na tatizo la udumavu wa kimo na akili.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi Februari 22, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Dk Germana Leyna wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kutathmini maendeleo ya Tanzania kuhusu ahadi zake katika mkutano wa kimataifa wa lishe na ukuaji (N4G).
Amesema mtoto aliyepata udumavu kutokana na kukosa lishe, bila hatua za haraka kuchukuliwa anaweza kupata athari za kudumu kitendo ambacho si sawa katika jamii, ndio maana Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi wamekuwa wakikutana mara kwa mara kuhakikisha suala la udumavu linatokomezwa
“Hatua mbalimbali zinachukuliwa na Serikali kwa ajili ya kukabiliana na udumavu Kwa watoto, lakini pia kuhakikisha jamii inafuata taratibu za uandaaji wa lishe bora,” amesema Dk Leyna.
Hata hivyo, amesema upungufu wa vitamini na madini ambavyo ni sehemu ya lishe vinachangia udumavu kwa watoto, hivyo jamii inapaswa kuvizingatia katika uandaaji wa lishe.
Amesema visababishi hivyo vimekuwa vikiathiri pia wanawake walio katika umri wa kuzaa, kutokana na changamoto ya utapiamlo uliozidi uzito, ambapo kwa takwimu za mwaka 2022 zinaonyedha kuwa asilimia 37 ya wanawake wana uzito uliozidi, wakati wanaume waliozidi umri ni asilimia 17.
“Moja ya mikakati tuliojiwekea katika majadiliano yetu ni kuhakikisha hadi ifikapo 2030 Tanzania imeondokana na tatizo hili la utapiamlo,” amesema Dk Leyna.
Amesema kiwango cha unyonyeshaji kwa akina mama kimeongezeka kutoka asilimia 50 hadi asilimia zaidi ya 70 kitendo ambacho kinaonyesha kuna kazi kubwa inafanyika katika kuhakikisha jamii inatekeleza kwa asilimia kubwa masuala ya lishe.
Kwa upande wake msimamizi kiongozi wa Afya na Lishe kutoka World Vision Tanzania, Elizabeth Ndaba amesema moja ya nyanja ambazo inatekeleza katika maeneo mbalimbali ni pamoja na kwenye kukabiliana na utapiamlo kwa watoto, katika elimu pamoja na sekta ya afya ambapo wamekuwa wakitoa afua mbalimbali ambazo zinasaidia jamii.
“Shirika limekuwa likishirikiana na Serikali katika nyanja mbalimbali, ikiwemo utekelezaji wa N4G katika ahadi ambazo Serikali imejiwekea” amesema Ndaba.
Ameongeza kuwa World Vision itaendelea kushirikiana na serikali kupitia mradi wao wa Inatosha unaolenga kupunguza tatizo la utapiamlo katika maeneo mbalimbali Nchini.
Source: mwananchi.co.tz