Dar es Salaam. Tanzania inakusudia kutangaza jina la Dk Faustine Ndugulile kuwania nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Gazeti la Mwananchi limebaini.
Kazi ya kunadi jina la Dk Ndugulile kuwa mteule wa Tanzania katika nafasi hiyo, itaanza rasmi leo katika hafla ya kumtangaza itakayofanywa na uongozi wa Wizara ya Afya na ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Vyanzo vya habari kutoka Wizara ya Afya vililiambia Mwananchi kuwa Dk Ndugulile, ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Afya, ndiye atakayeshindanishwa na wagombea wengine kutoka nchi nyingine kuwania nafasi hiyo.
“Tanzania imemchagua Dk Ndugulile kuwa Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika na tangazo rasmi litatolewa kesho,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, Dk Ndugulile hakupatikana alipotafutwa jana kuzungumzia suala hilo.
Iwapo azma ya Tanzania ya kuwania nafasi hiyo itakamilika, Dk Ndugulile ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Kigamboni, jijini Dar es Salaam, kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) atachukua nafasi ya Dk Matshidiso Moeti kutoka Botswana, ambaye muda wake unamalizika Agosti mwaka huu baada ya kuhudumu katika nafasi hiyo tangu mwaka 2015.
Kwa kuwa Ofisi ya Kanda ya Afrika ya WHO ipo huko Brazzaville, Jamhuri ya Kongo huenda inaweza kuwa changamoto kwa Dk Ndugulile kama atapata nafasi hiyo kuendelea na nafasi yake ya ubunge wa kuwatumikia wananchi wa Kigamboni.
Kazi kubwa ya kiongozi na Mkurugenzi wa Kanda ni kukuza ushirikiano na washirika wa ndani ya Afrika na nje kwa maana ya waliokuwepo na wapya, ikijumuisha taasisi za uhisani, asasi za kiraia, wasomi na kuongeza ushirikiano kati ya vijana na wanawake katika afya kimataifa.
Kufutia kuteuliwa huko, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Deus Ndilanha alisema Dk Ndugulile kupata nafasi ya kuwania ni jambo kubwa kwa tasnia ya tiba, lakini pia ni mafanikio makubwa kwa nchi iwapo atapata hiyo nafasi.
“Dk Ndugulile ni daktari mwenzetu na tulikuwa naye kwenye mkutano wetu mwaka jana jijini Tanga, unapoona daktari mwenzio anapata nafasi hiyo ni heshima kwetu kututangaza, dunia itajua Tanzania ina watu wazuri wanaoweza kuongoza mataifa mengine, tunamuombea kila la heri,” alisema Dk Ndilanha.
Dk Ndugulile ni nani?
Dk Ndugulile ni daktari mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 25 kwenye afya ya jamii ndani na nje ya nchi. Amewahi kuwa mwakilishi wa Bara la Afrika katika Taasisi ya kimataifa ya Ukimwi na mwanzilishi wa mtandao wa dunia kuhusu ugonjwa wa TB.
Pia, amewahi kuwa Naibu Waziri wa Afya na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari hapa nchini.
Machi 11, 2023, Dk Ndugulile aliteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya ushauri masuala ya afya ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU). Rais wa IPU ni Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson.
Kwa uteuzi huo, unaofanywa na Rais wa umoja huo wa mabunge duniani, ulimfanya Dk Ndugulile kuwa sehemu ya wabunge 12 duniani wanaoishauri IPU kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu afya.
Uteuzi huo ulianza Februari mwaka 2023 ambao utadumu kwa miaka minne. Oktoba 24, 2023 Dk Ndugulile alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati ya ushauri ya masuala ya afya ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika uchaguzi uliofanyika Luanda, nchini Angola.
Kamati ya ushauri ya masuala ya afya, ina majukumu ya kushauri mabunge ya nchi na umoja wa mabunge duniani kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu afya.
Pia, katika uchaguzi huo, Seneta Lorraine Clifford-Lee wa Ireland alichaguliwa kuwa Mwenyekiti, huku wajumbe wengine wa kamati hiyo wakitoka nchi za Mexico, Croatia, Cuba, Pakistan, Russia, Saudi Arabia na Uzbekistan.
Katika mkutano huo, Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson alichaguliwa kuwa rais wa IPU Oktoba 27, 2023.
Source: mwananchi.co.tz