Dk Mollel: Hakuna mgonjwa yeyote wa homa ya nyani Tanzania

Dk Mollel: Hakuna mgonjwa yeyote wa homa ya nyani Tanzania

Morogoro. Imeelezwa kuwa hadi sasa hakuna mgonjwa aliyethibitika kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa homa ya nyani (Mpox) nchini Tanzania hivyo wananchi wanatakiwa kutokuwa na hofu bali waendelea kuchukua tahadhari.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Agosti 28, 2024 na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel kwenye hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa Chama cha Wateknolojia Dawa na Wateknolojia Dawa Wasaidizi (TAPHATA) uliofanyika mkoani Morogoro.

Dk Molle amesema Agosti 17, mwaka huu, Wizara ya Afya ilitoa taarifa kwa umma kuhusu ugonjwa huo kufuatia ongezeko la visa duniani, ikiwemo baadhi ya nchi za Afrika Mashariki na kuutahadharisha umma kuchukua hatua za kuzuia ugonjwa huo kuingia nchini.

Pamoja na tahadhari hiyo, amewataka wataalamu wa afya na wateknolojia dawa kutoa elimu na kushirikiana na jamii kuhakikisha nchi inabaki salama.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amesema ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2018 ilibainisha kuwa ifikapo mwaka 2050, watu zaidi ya milioni 10 watafariki dunia kila mwaka kutokana na magonjwa yanayotokana na vimelea sugu kutokana na utumiaji usio sahihi wa dawa.

Hivyo amesisitiza kuwa Serikali inaongeza juhudi za kusimamia matumizi sahihi ya dawa ili kupunguza madhara yanayotokana na matumizi yasiyo sahihi, hasa za aina ya antibiotiki.

“Ni jukumu lenu wataalamu wa famasia kuchukua hatua sasa katika mapambano dhidi ya usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa. Hakikisheni mnatoa elimu sahihi kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya dawa kwa kuwa ninyi ndio kada ya afya inayohusika zaidi,” amesema Mollel.

Ameagiza mamlaka na mabaraza yanayosimamia huduma za dawa na tiba nchini kuhakikisha maduka yote ya dawa yanasajiliwa na kukaguliwa mara kwa mara pamoja na vituo vyote vya afya vya umma na binafsi kuwa na wataalamu stahiki.

Kwa upande wake, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi amewataka wateknolojia dawa kufanya kazi kwa weledi ili kuepuka kazi hizo kufanywa na kada nyingine zisizo na utaalamu.

“Nina kesi moja iliyotokea wiki mbili zilizopita hapa Morogoro; kuna zahanati (jina limehifadhiwa) yenye stoo ya dawa lakini haina mtaalamu wa dawa. Nimeitaka zahanati hiyo itafute mtaalamu wa dawa, vinginevyo tutachukua dawa zetu kwa kuwa hakuna mtaalamu mwenye taaluma,” amesema Msasi.

Pia, amekemea tabia ya baadhi ya wafamasia kufungasha dawa kwenye bahasha zisizo rasmi na kuwataka wataalamu kuwa na kauli nzuri kwa wagonjwa na kuhakikisha dawa zinapatikana.

Rais wa Taphata, Thabiti Milandu amesema usugu wa dawa unasababishwa na mambo mbalimbali kama utumiaji holela wa dawa, kutomaliza dozi, na matumizi ya dawa za binadamu kwa kutibu wanyama.

Amesema wataalamu wa dawa wanatoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari na makongamano lengo likiwa kupunguza athari za matumizi holela.

Baadhi ya wafamasia wa Morogoro walisema wanakutana na changamoto wakati wa kuhudumia wagonjwa, huku Eda Abdul akieleza kuwa baadhi ya wagonjwa wanapendelea dawa wanazotaka wao, na si zile zilizoandikwa na daktari, jambo linalosababisha matumizi mabaya ya dawa.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories

Top News
Investment News Editor

ZSSF money not for projects, says Ali Karume

Unguja. Veteran politician and diplomat Ali Karume has called on authorities of the Zanzibar Revolutionary Government (SMZ) to refrain from using the Zanzibar Social Security Fund money for establishing commercial projects.Continue Reading