Unguja. Uchumi wa nchi yoyote unategemea zaidi miundombinu bora, kurahisisha usafiri na usafirishaji.
Miongoni mwa miundombinu hiyo ni ya barabara nzuri, imara zenye alama kwa kujali watumiaji wote.
Zanzibar licha ya kuwa na miundombinu ya barabara, bado ina safari ndefu ya kuziwezesha kuwa na sifa hiyo.
Kuna mambo yanaonekana kama madogo lakini athari yake ni kubwa, ikiwamo watu kupoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa kudumu.
Mara kadhaa kumekuwa na ajali zinazotokana na uzembe wa madereva, ufinyu wa barabara, ukosefu wa vituo maalumu vya kupakia na kushusha abiria, na kutokuwapo alama za barabarani.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali (OCGS) kwa mwaka 2023 jumla ya ajali 193 zimeripotiwa, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi ikiripotiwa kuwa na ajali zaidi ambazo ni 31 sawa na asilimia 16.6 ikilinganishwa na wilaya nyingine.
Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 12.2 kutoka ajali 172 kwa mwaka 2022.
Wilaya inayofuata ni ya Kati, Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa na ajali 31; Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja (22); Wilaya ya Magharibi B (22); Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba (19) na Kaskazini A (16).
Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja (13); Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini (11); Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba (10); Wilaya ya Mkoani Kusini Pemba (10); na Wilaya ya Mjini (7).
Kutokana na ajali hizo, watu 385 wameripotiwa kupoteza maisha kati ya hao, 343 walikuwa wanaume na 42 wanawake.
Kwa mujibu wa OCGS, hilo ni ongezeko la asilimia 19.2 kutoka watu 323 waliofariki dunia mwaka 2022.
Waliojeruhiwa wameongezeka kwa asilimia 12.5 kutoka waathirika 136 mwaka 2022 hadi kufikia majeruhi 153 mwaka 2023.
Wilaya ya Magharibi A, imeripotiwa kuwa na waathirika wengi ambao ni 58 sawa na asilimia 15.1 ikilinganishwa na wilaya zingine.
Kwa Mujibu wa OCGS, waathirika 151 (waliofariki dunia na kujeruhiwa) walikuwa abiria, wapanda baskeli na pikipiki ni 130 na waenda kwa miguu 78, huku madereva walikuwa 26.
Jumla ya makosa 38,598 yameripotiwa, kati ya hayo 38,522 yameripotiwa kwa wanaume na 76 yakiwa ya wanawake.
Kosa kubwa lililoripotiwa ni kutofuata miongozo na kanuni za usalama barabarani ambayo ni 12,419.
Ajali za miezi miwili ya Januari na Februari 2024 ni 41.
Kwa Januari pekee, kuna ajali 22 na Februari 19. Hata hivyo, zimeongezeka kwa asilimia 46.2 ikilinganishwa na ajali 13 kwa Februari 2023. Januari zimeongezeka asilimia 22.2 ikilinganishwa na 18 za Januari 2023.
Maoni ya wananchi
Wakizungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi, madereva na wadau wa barabara wamekuwa na mitazamo tofauti, zaidi wakiibua changamoto zinazochangia ajali, wakitaka ziangaliwe kwa jicho la pekee kumaliza matatizo hayo.
Uzembe unatajwa na wengi kuchangia ajali. Mengine yakiwa ukosefu wa alama za barabarani, vituo vya daladala na ufinyu wa barabara.
Barabara nyingi hususani za mjini hazina vituo maalumu vya daladala, badala yake magari husimama barabarani wakati wa kupakia na kushusha abiria.
“Angalia barabara zote hizi za mjini hazina vituo vya daladala, zinashusha na kupakia njiani, labda tu kwa kukariri kwamba eneo fulani kuna kituo lakini kiuhalisia hakuna kituo kilichoandaliwa maalumu kwa kazi hiyo,” anasema Burhan Othman, mkazi wa Magomeni.
Dereva wa daladala linalofanya safari kati ya Mjini na Bububu, Suleiman Moh’d amesema miundombinu ya barabara hiyo, upana wake na wingi wa magari yanayoingia na kutoka haviendani, hivyo mbali na kusababisha foleni hata ajali zimekuwa zikitokea.
“Pamoja na makosa mengine ya madereva, lakini yapo ambayo yanasababishwa na miundombinu, kwa hiyo mamlaka lazima ziangalie jambo hili na athari zake,” amesema.
Abdulla Njau amesema, “nenda kaangalie mazingira ya Tobo la Pili (kituo kikuu cha daladala eneo la nyumba za Michenzani) hakuna maegesho ya daladala badala yake zinaegeshwa kando mwa zingine zinashusha na kupakia barabarani, mazingira kama haya si tu yanaleta foleni lakini yanasababisha ajali.”
Mkazi mwingine, Fauzia Ali anaeleza kutokuwapo alama za barabarani, zikiwamo za vivuko vya waenda kwa miguu (pundamilia) kunachangia ajali.
“Binafsi nimeshuhudia kwa macho yangu eneo la Darajani huwa kuna zebra (kivuko cha waeda kwa miguu) lakini muda mrefu zilishafutika kwa hiyo hata magari yakifika hayasimami lakini wananchi wanavuka. Ajali zimekuwa zikitokea kwa sababu ya mwingiliano huo,” anasema Ali.
Kauli za mamlaka
Askari wa Usalama Barabarani akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina anakiri miundombinu huwapa changamoto ya usimamizi wa sheria.
“Unaweza kuliona kwamba hili ni kosa, gari linapakia abiria barabarani, utatoa amri na kuonya lakini wakati mwingine unaangalia huoni namna ambavyo dereva angefanya. Kwa kweli hiyo ni changamoto,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud amesema ongezeko la ajali wakati mwingine linachangiwa kwa kiasi kikubwa na tatizo la miundombinu na si madereva wala vyombo vya usafiri kama ambavyo inatajwa na kuelezwa.
“Mara nyingi linapozungumzwa suala la usafiri na usafirishaji, tumekuwa tukitazama vyombo badala ya kuitazama miundombinu. Wakati mwingine ongezeko la ajali linatokana na changamoto ya miundombinu na si madereva wala vyombo vya usafiri,” amesema Mahmoud.
Amesema Serikali ina wajibu wa msingi kuona sekta ya usafiri na usafirishaji inavyoweza kusaidia usalama wa wananchi.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, yamefanyika maboresho makubwa ya kisera, kisheria na kikanuni kutoa mazingira wezeshi katika sekta ya usafirishaji.
Amesema ipo haja ya kubaini barabara zenye kasoro na alama za barabarani zilizokosewa.
“Mfano barabara inayotoka Mjini Unguja kueleka Nungwi, Mkoa wa Kaskazini, imejengwa si zaidi ya miaka mitano nyuma, lakini ukiangalia upana wake na wingi wa magari yanayopita katika barabara hiyo, inaweza ikawa changamoto na hilo linachangia ongezeko la ajali,” amesema Mahmoud.
Mfano mwingine anasema ni barabara ya Tunguu-Makunduchi, Paje-Michanvi, akieleza kasi ya watu na ongezeko la uwekezaji katika Mkoa wa Kusini Unguja haviendani na hali ya miundombinu ya barabara hizo.
Amesema kasi ya watu na vyombo vya usafiri vyote viwe sehemu ya viashiria wakati wa kusimamia miundombinu ya usafiri na usafirishaji ili kuwe na uwiano kati ya ongezeko la watu na miundombinu ya usafirishaji.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, iwapo vitu hivyo vikiangaliwa kwa upana wake; ajali za barabarani zitapungua.
Mkuu wa Usalama Barabarani Kamisheni ya Zanzibar, Shida Machumu amesema yapo mambo mengi ambayo inawezekana maofisa wa kusimamia usalama hawayajui.
Amesema barabara zinaweza kuwa hazina viwango na zimekosewa katika ujenzi.
Machumu amesema barabara nyingi ni za zamani, hivyo ni finyu na vyombo vya moto vinaongezeka ilhali barabara hazina sehemu za watembea kwa miguu.
Ameshauri zinapojengwa barabara mpya kuhakikisha matakwa yote yanazingatiwa.
Kuhusu madereva, amesema licha ya ubovu wa miundombinu hiyo, hawana kipaumbele kwa madereva wenzao bali wanaendesha gari kana kwamba wapo porini.
“Hata akiona sehemu haina miundombinu mizuri wao hawazingatii hilo, hili ndilo linaongeza hizo ajali. Kwa hiyo ipo haja ya elimu kuendelea kutolewa, na kila upande kutimiza wajibu wake,” amesema.
Katika hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya mwaka 2023/24 ambayo iliwasilishwa na Waziri mwenye dhamana, Dk Khalid Salum Mohamed, changamoto ya uhaba wa fedha inakwamisha uwekaji wa michoro na alama za barabarani.
Wizara kupitia Wakala wa Barabara Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2022/23 ilipanga kuweka alama na michoro ya usalama barabarani katika maeneo tofauti Unguja na Pemba.
Ilipanga kutumia Sh80 milioni kwa ajili ya kuweka alama za usalama barabarani Unguja lakini hakuna fedha iliyopatikana kwa ajili ya shughuli hiyo.
Hata hivyo, Waziri Khalid anasema kutokana na ujenzi wa barabara mpya unaoendelea vitu hivyo vitazingatiwa.
Source: mwananchi.co.tz