Zanzibar. Zanzibar inakabiliwa na changamoto za kimazingira, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa kina cha bahari, uvamizi wa maji ya chumvi, mmomonyoko wa fukwe, na hali mbaya ya hewa.
Ofisa Uratibu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu, Omar Mohamed, ameeleza changamoto hizo Machi 10, 2025 wakati wa warsha kuhusu uchumi rejelezi (Circular Economy) na Uchumi wa Buluu iliyoandaliwa na Afrika 21 kwa kutanisha waandishi wa habari, wataalamu wa uchumi relejezi na uchumi wa buluu kutoka Afrika, hususan mataifa ya pwani na visiwa vya Bahari ya Hindi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Hamad Bakar Hamad akizungumza na waandishi wa habari
Omar Mohamed amebainisha kuwa uharibifu wa miamba ya matumbawe unatishia sekta za uvuvi na utalii, huku uvamizi wa maji ya chumvi na mabadiliko yasiyotabirika ya mvua yakihatarisha kilimo na vyanzo vya maji safi.
“Tunahitaji kuchukua hatua sasa ili kulinda maisha na usalama wa chakula,” amesema akiongeza miongoni mwa madhara ni jamii za pwani zikilazimiaka kuhama kwa lazima kutokana na kupungua kwa ardhi.
Amesema asilimia 23 hadi 54 ya watu wanakabiliwa na tatizo hili. Aidha, kupungua kwa idadi ya samaki kumeathiri ustawi wa wavuvi, hivyo kuhatarisha riziki na usalama wa chakula.
Akifafanua zaidi, amesema, “tafiti na shuhuda za wavuvi zinaonyesha kupungua kwa mazalia ya samaki, hali inayolazimisha Serikali kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha sekta ya uvuvi.”

Umuhimu wa uhifadhi wa mazingira
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Hamad Bakar Hamad, amesisitiza kuwa uchumi wa Zanzibar unategemea sana bahari, huku sekta za uvuvi na utalii zikiwa nguzo kuu za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Sekta hizi zinategemewa na takriban theluthi mbili ya wakazi wa Zanzibar, huku uvuvi ukichangia kati ya asilimia nne hadi 8 ya Pato la Taifa (GDP) na utalii ukichangia zaidi ya asilimia 29,” amesema Hamad.
Tasnia nyingine muhimu ni pamoja na ufugaji wa baharini, kilimo cha mwani, na uvunaji wa holothuria (sea cucumbers), ambavyo vina mchango mkubwa katika uchumi wa Zanzibar.
Mwaka 2024, uzalishaji wa mwani ulifikia takriban tani 18,000, huku asilimia 99 ya biashara za kimataifa zikitegemea rasilimali za bahari.

Licha ya mchango huu wa kiuchumi, Hamad amekiri kuwa Zanzibar inakabiliwa na changamoto za uendelevu, akihimiza mabadiliko ya mbinu za matumizi ya rasilimali ili kuhakikisha manufaa ya muda mrefu kwa mazingira na jamii.
Hatua zinazochukuliwa
Katibu Mkuu Hamad amesema Serikali inawahamasisha wanawake wanaojihusisha na kilimo cha mwani pamoja na wavuvi kuhamia maeneo ya kina kirefu cha bahari ili kulinda akiba ya samaki na kuongeza mavuno.
“Ili kuwezesha mabadiliko haya, Serikali imewapatia wavuvi na wakulima wa mwani zaidi ya boti 1,000 kwa riba ya asilimia 0,” amesema.
Aidha, amebainisha wanafanya jitihada kutafuta masoko bora na kuanzisha viwanda vya usindikaji ili kuimarisha mnyororo wa thamani wa bidhaa zinazozalishwa.
“Mkakati wetu unahakikisha kuwa wanawake hawaachwi nyuma katika shughuli zao za kiuchumi, bali wanapewa nyenzo na fursa za kustawi katika Uchumi wa Buluu. Wizara yetu imejizatiti kuwasaidia wanawake kuendelea kushiriki kikamilifu katika sekta hii,” amefafanua.
Amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali katika uhifadhi wa mazingira na uwezeshaji wa kiuchumi inalenga kuhakikisha kuwa rasilimali za bahari za Zanzibar zinaendelea kunufaisha jamii huku zikihifadhiwa kwa vizazi vijavyo.
Ili kukabiliana na changamoto hizi, Omar Mohamed amependekeza kupanua uchumi wa buluu kupitia kilimo cha mwani na bioteknolojia ya baharini, kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala, na kutekeleza miradi ya kulinda fukwe.
Pia amesisitiza umuhimu wa utalii endelevu na kuwawezesha vijana kwa ujuzi wa uhifadhi wa mazingira na mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Source: mwananchi.co.tz