
Mbeya. Chama cha Kutetea Haki na Masilahi ya Walimu Tanzania (Chakamwata) kinatarajia kumuona Rais Samia Suluhu Hassan kujadili masuala mbalimbali kuhusiana na haki na masilahi ya walimu nchini.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Meshack Kapange amesema hayo leo Alhamisi Machi 6, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio mpya huku akisisitiza wataanza na vita ya kikokotoo.
Kapanga amesema Februari 8, 2020 ofisi ya msajili wa vyama vya wafanyakazi na waajiri aliwaandikia barua ya kuondoa jina la Chakamwata na kukifutia usajili.
Hatua hiyo ilisababisha chama hicho kutafuta haki kwa kufungua shauri namba 1/2020 katika Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.
Kufuatia mwenendo wa kesi walikata rufaa na shauri hilo kusikilizwa katika Mahakama ya Rufani ambayo Februari 27, 2025 ilitoa amri ya hukumu ya kurejeshewa usajili wa chama baada ya kukaa kifungoni kwa miaka sita iliyopita.
Katika mkutano huo na waandishi, Kapange amesema: “Wakati wowote tunatarajia kumuona Rais Samia Suluhu Hassan na wizara husika kuzungumzia ajenda mbalimbali zinazohusu masilahi ya walimu na wafanyakazi nchini baada ya kusota miaka sita kushindwa kupaza sauti.”
Kapange amesema wamejipanga kuanza kwa nguvu mpya kupaza sauti kutetea haki za walimu na wafanyakazi kwa kusimamia ajenda ya kupinga kanuni mpya ya mafao ya kikokotoo cha wastaafu nchini.
“Katika kutimiza hayo matarajio yetu kupata ushirikiano mkubwa serikalini ili kufikia ajenda zetu kwa masilahi ya wafanyakazi nchini,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama hicho, Ipyana Kabuje amesema kazi kubwa iliyo mbele yao ni kuona namna gani wanafikia malengo waliyoshindwa kuyafikia kipindi cha miaka mitano iliyopita.
“Tunaendeleza tulipoishia, huu ni moto mwingine wa kutetea haki na masilahi ya walimu na wafanyakazi nchini,” amesema.
Source: mwananchi.co.tz