Wapata dawa ya utoro, mimba kwa wanafunzi wa kike

Mufindi. Ili kupunguza utoro na mimba kwa wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari Ilongo iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Mufindi, Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), kupitia shamba la miti la Sao Hill wametoa vifaa vya ujenzi wa bweni la wasichana vyenye thamani ya zaidi ya Sh30 milioni kwa ajili ya ujenzi wa bweni hilo.

Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo leo Juni 29, 2024, Ofisa Elimu Sekondari Wilaya Mufindi, Daniel Mapilya amesema msaada huo uliotolewa na Sao Hill, una manufaa katika kupunguza viashiria hatarishi vya mimba kwa watoto wa kike shuleni.

“Wanafunzi hawa walikuwa wanapanga mitaani kwenye nyumba za wananchi bila kuwa na uangalizi wa aina yoyote, hivyo msaada huo wa vifaa vya kujenga bweni kutoka Sao Hill utawasaidia kusoma kwa pamoja wakiwa bwenini bila usumbufu wowote,” amesema Mapilya.

Amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa bweni hilo, litawasaidia wanafunzi wao kwa kuwapunguzia kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilometa nane hadi kufika shuleni hapo.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ikweha, Tabia Chibwana amesema uwepo wa bweni hilo utasaidia kupunguza changamoto ya watoto wa kike kupata ujauzito, hivyo litasaidia watoto hao kutimiza ndoto zao.

Ofisa huyo amesema shule hiyo ina zaidi ya wanafunzi 448, kati yao 268 ni wanafunzi wa kike ambapo tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 2007, wamekuwa wakipata changamoto ya wanafunzi hao kurubuniwa, hali ambayo imesababisha kupata ujauzito kwa sababu ya kukaa mitaani kwenye vyumba vya kupanga.

Mhifadhi Mkuu wa Sao Hill, Yebby Yoram amesema wataendelea kusaidia kadri bajeti itakavyokuwa kusaidia miradi kama hiyo katika maeneo mengine.

“Maombi mengi yanahusu miradi kama hii lakini kuna baadhi ya shule tumesaidia miradi hiyo ikiwemo shule ya sekondari Luganga, Changalawe pamoja na shule zingine,” amesema.

Awali akisoma taarifa ya vifaa hivyo, Mhifadhi Mwandamizi wa shamba la Sao Hill, Peter Nyahende amesema Sao Hill wanatambua umuhimu wa mazingira bora ya kutolea elimu kwa watoto hao kwa kukabidhi vifaa hivyo kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana katika shule hiyo.Continue Reading

Pingamizi mgombea ADC lapuuzwa, wanachama 197 kuamua

Dar es Salaam. Wakati wapiga kura 197 wakitarajia kufanya uamuzi wa kikatiba kumchagua mwenyekiti mpya wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Kamati ya uchaguzi huo imesema pingamizi alilowekewa mmoja wa wagombea wa nafasi ya mwenyekiti, Shabani Haji Itutu halijafuata kanuni za chama.

Itutu aliwekewa pingamizi na wanachama saba wa ADC, Ibrahim Pogora, Asha Milongea, Asha Mzee, Khadija Tambwe, Maisala Khamis, Doni Mnyamani na Halima Msumali wakidai ni mwanachama wa chama kingine cha upinzani.

Katibu wa kamati ya uchaguzi, Innocent Siriwa ameiambia Mwananchi Digital leo Ijumaa, Juni 28, 2024 kwamba wamepokea pingamizi hilo, lakini kwa mujibu wa kanuni za chama, kamati haitalifanyia kazi.

“Kwanza limekuja nje ya muda wa mapingamizi uliowekwa, lakini pia kanuni za chama zinaelekeza mtu anayetakiwa kumwekea pingamizi mgombea ni mgombea mwingine, sio wanachama,” amesema Siriwa.

Akizungumzia mchakato wa uchaguzi huo utakaofanyika kesho Jumamosi, Siriwa amesema mkutano mkuu utaanza saa 2:00 asubuhi na wanatarajia mchakato wote hadi kupata viongozi wapya wa ADC kukamilika saa 10:30 jioni kwenye hoteli ya Lamada, Ilala jijini Dar es Salaam.

“Wapiga kura ni 197 kutoka Bara na Zanzibar, wataanza kwa kumchagua mwenyekiti (nafasi hiyo inawaniwa na Itutu aliyewahi kuwa makamu mwenyekiti na Doyo Hassan Doyo aliyewahi kuwa katibu mkuu), mshindi atakabidhiwa madaraka na mwenyekiti anayemaliza muda wake (Hamad Rashid).

“Atakapokabidhiwa, mwenyekiti mpya ndiye ataendelea na mchakato wa kuwapata makamu mwenyekiti wa Bara na Zanzibar,” amesema Siriwa.

Wanaowania nafasi hiyo upande wa Bara ni Scola Kahana na Hassan Mvungi na Zanzibar ni Fatma Salehe na Shara Amrani huku pia kesho utafanyika uchaguzi wa nafasi 19 za wajumbe Bodi ya uongozi taifa.

Kwa mujibu wa Siriwa, nafasi hizi wagombea wake watachukua na kurudisha fomu siku hiyohiyo ya uchaguzi (kesho), watapigiwa kura siku hiyo ukumbini na kati ya watakaochaguliwa, robo au nusu ya idadi hiyo wanapaswa kutoka Zanzibar.

Kabla ya uchaguzi huo kesho, leo Ijumaa kuanzia saa moja usiku, Bodi ya Taifa ya uongozi ya ADC itakuwa na mkutano mkuu maalumu kupitisha ajenda za mkutano huo mkuu wa uchaguzi.

“Mkutano mkuu unatambuliwa na Bodi ya taifa ya uongozi, ambayo ndiyo itapitisha ajenda za mkutano mkuu wa kesho,” amesema Siriwa.

Kampeni za uchaguzi wa chama hicho zitakoma leo saa 12 jioni ambapo zitafungwa tayari kwa uchaguzi huo kesho, huku wagombea wakisisitizwa kufuata kanuni na taratibu za chama ambazo zimeelekeza kufanya kampeni za kukijenga na kugusa maisha ya wananchi.Continue Reading

Kariakoo ngoma mbichi

Licha ya Serikali kutangaza kuwa itafanyia kazi malalamiko ya wafanyabiashara wa Kariakoo, ikiwemo kusitisha kamatakamata iliyokuwa ikifanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), baadhi ya wafanyabiashara wamesema Rais Samia Suluhu Hassan ndiye anapaswa kutoa tangazo hilo..Continue Reading

‘Msiwe kikwazo wakimbizi kurejea nchini mwao’

Kibondo. Mashirika ya kuhudumia wakimbizi yaliyopo mkoani Kigoma yametakiwa kutokuwa kikwazo kwenye makubaliano yaliyowekwa na serikali za Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR), ya kuhamasisha wakimbizi kujiandikisha na kurejea nchini mwao kwa hiari.

Hayo yamebainishwa Juni 20, 2024 wilayani Kibindo na Mkurugenzi wa Idara ya Wakimbizi nchini, Sudi Mwakibasi wakati wa maadhimisho ya siku ya mkimbizi duniani yaliyofanyika katika kambi ya wakimbizi ya Nduta.

Amesema Serikali ya Tanzania inasimamia makubaliano hayo na hivyo kila mmoja anapaswa kutekeleza badala ya kuwa kikwazo.

“Kinachofanyika ni kupambania maslahi binafsi na taasisi , wakati Serikali inapambania maslahi ya watu wake na ya Warundi. Sasa haiwezekani Serikali kuumiza wakimbizi kwa sababu ya ajira, naombeni tuwasaidia wakimbizi kurejea nyumbani ili watumie fursa ya kwenda kujenga nchi yao,” amesema Mwakibasi.

Amesema ni vema viongozi wa kambi zote mbili na vyombo vya ulinzi na salama kuhakikisha vijana wa kiume kutotoka ndani ya kambi bila kibali maalumu kwani ni kinyume cha sheria na taratibu zilizopo kwani Serikali haijui wanaenda wapi na kufanya nini.

Mwakilishi wa Shirika la UNHCR nchini Tanzania, Mahoua Parums amesema kama hali inaruhusu wakimbizi hao anapenda kuwahamasisha kuangalia suluhisho la kudumu la urejeaji kwa hiari nchini mwao.

“Ndio tuna masuluhisho mengine lakini nyumbani ni nyumbani, hivyo ni vema kama hali inaruhusu waweze kurejea nyumbani kwa hiari na kwenda kuijenga nchi yao, jambo ambalo ni zuri na linaleta faraja,” amesema Parums.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Kanali Aggrey Magwaza amesema hadi sasa wakimbizi ambao wamesharejea nchini kwao kwa hiari ni 170,000 huku wakimbizi waliopo hadi sasa kwa kambi ya Nduta na Nyarugusu wakifikia 246,000.

Nao baadhi ya wakimbizi wa kambi ya Nduta, wamesema wanaendelea kujiandikisha ili waweze kurejea nchini kwao kwa hiari, na kwamba hakuna mwananchi anayeweza kuikimbia nchi yake bila sababu na kwenda kuwa mkimbizi kwenye nchi nyingine.

Mkimbizi Donatha Nibiza amesema Serikali ya Tanzania inatekeleza shughuli ya kuwarudisha nyumbani kwa hiari wakimbizi nchini kwao, lakini kila mkimbizi amekimbia kwa sababu zake maalumu, hivyo ni muhimu kuchukua hatua ya kuwasikiliza kwanza na kujua sababu zipi hasa zilizowafanya waweze kukimbia nchini kwao.

Iveti Nibaruza amesema yeye yupo tayari kurejea nchini kwake kwa hiari na kwamba muda wa promosheni uliotolewa na pande zote, anauunga mkono na atatumia kipindi hicho kwenda nchini kwake kuijenga nchi yake.Continue Reading