Wataalamu wapendekeza udhibiti bidhaa za mafuta Tanzania
Dar es Salaam. Wataalamu wa afya nchini Tanzania wamependekeza udhibiti wa uingizwaji wa mafuta na bidhaa zake, kama mbinu ya kuepuka magojwa yasiyo ya kuambukiza kwa wananchi.
Mafuta waliyopendekeza yadhibitiwe ni yale yasiyoandaliwa vizuri na yenye hatari kubwa kwa matumizi ya binadamu.
Sambamba na hilo, wataalamu hao wamesema kama inawezekana itafutwe namna ya kuongezwa kodi kwa aina hiyo ya mafuta, wakati yale yaliyo salama yapunguziwe kodi.
Wataalamu hao wamesema hayo leo, Jumatatu Julai 8, 2024 walipokuwa wakichangia kwenye mjadala wa Mwananchi Space, uliojadili ‘Ulaji wa vyakula vya mafuta mengi na athari zake ulioandaliwa kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC).
Ofisa Lishe na Mtafiti Mwandamizi TFNC, Maria Ngillisho amesema vyakula vinavyopikwa kwa mafuta mengi vinavutia na vitamu, lakini vina madhara makubwa mwilini.
Amesema kupika kwa mafuta ni njia rahisi, lakini ina athari kiafya hasa vyakula hivyo vikitumiwa kwa wingi na mara kwa mara.
“Tuna vyakula tunavyopika kwenye mafuta mengi na hivi tunaweza kuviepuka kwa kupika kwa kutumia mbinu nyingine ikiwemo kuoka,” amesema.
Maria ameeleza vyakula vyenye mafuta mengi ni vile vyenye asili ya mafuta na vinavyopikwa kwa mafuta mengi.
Amevitaja vyakula hivyo ni karanga, mbegu za alizeti, korosho na vile vyenye asili ya mimea.
Naye Mkuu wa kitengo cha Utafiti na daktari bingwa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Pedro Pallangyo amesema kiwango kikubwa cha mafuta kinasababisha mwili ushindwe kuyatumia katika shughuli za kawaida.
Hatua hiyo, amesema inasababisha yajihifadhiwe sehemu mbalimbali na hivyo kusababisha magonjwa.
“Dalili ya kuakisi kuwa mafuta ni namna anavyoongezeka uzito, kiribatumbo na mabadiliko hayo yanakuwa ndani ya mili yetu, hasa mafuta yanapoingia katika mfumo wa moyo na mishipa ya damu,” amesema.
Amesema binadamu walivyoumbwa mili yao ina mishipa ya damu yenye upenyo mdogo ambao damu inapita na ukubwa wake ni sahihi katika kukidhi mahitaji.
“Mafuta yakitanda katika mishipa mikubwa ya damu ukubwa wake unapungua, sasa inategemeana imetanda katika mishipa ipi ina maana hayo maeneo yatapokea kiwango kidogo cha damu kuliko inavyotakiwa,” amesema.
Amesema kutokana na wimbi la mafuta katika jamii hata vijana wanaanza kuonekana na magojwa hayo, huku akieleza wengi wanakuja na malalamiko ya magonjwa ya miguu na kuanza kubadilika rangi.
“Tafsiri ya haraka maeneo yaliyobadilika rangi hayapati kiwango cha damu ya kutosha na ukifanya uchunguzi wa miguu ya hao wahusika unaona mishipa midogo midogo inayolisha miguu inakuwa imeziba,” amesema.
Amesema kumekuwa na ongezeko la watu wengi kuziba mishipa mitatu ya moyo inayosababisha vifo vya ghafla kwa kuwa wanakosa hewa ya oskjeni kwenye moyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza wa Wizara ya Afya, Dk Omary Ubuguyu amesema kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, kwa mwaka Serikali huitaji Sh1.1 trilioni kukabiliana na magonjwa hayo.
“Sisi tukiangalia mkakati wetu wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza tunahitaji Sh1.1 trilioni kwa mwaka kutoa huduma stahiki kutoa huduma stahiki kwa magonjwa sawa na bajeti nzima ya Wizara ya Afya inayotolewa sasa,” amesema Dk Ubuguyu.
Dk Ubuguyu amesema nchi imefika katika kiwango cha ukubwa wa tatizo kwa sababu walichelewa kuanza kupambana na magonjwa hayo, kwani waliamini ni tatizo linalowapata zaidi watu wa ukanda wa Afrika Magharibi.
Naye Mtaalamu wa lishe wa TFNC, Elizabeth Lyimo amesema mafuta ni moja ya kundi la chakula lenye kazi maalumu mwilini kutokana na virutubisho vilivyopo.
“Kundi hili linapaswa liliwe kwa kuangaliwa kwa sababu linatoa kiwango kikubwa cha nishati lishe, laikini kuna aina mbili za mafuta ya kimiminika (yasiyo ganda) ni yale yanayotokana na mimea na yanayoganda yanatokana na wanayama,” amesema.
Awali, Mhariri wa Jarida la Afya Gazeti la Mwananchi, Herieth Makwetta akichokoza mada amesema ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi ni chanzo cha magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwemo shinikizo la damu na saratani.
“Utafiti wa mwisho uliofanywa na Wizara ya Afya mwaka 2018 unaonyesha asilimia 33 ya vifo vyote vilivyotokea nchini vilisababishwa na magonjwa yasiyoambukizwa,” amesema.
Katika maelezo yake Makwetta, amefafanua wataalamu wanaonya kuwa ifikapo mwaka 2027, huenda vifo vinavyotokana na hayo magonjwa vitafikilia asilimia 54.
“Wataalamu wanasema mafuta yanahitaji kiwango kidogo mwilini kwa kazi ya kumpatia nguvu kiasi cha dole gumba, lakini wengi wamekuwa wakikiuka na kujikuta wakiongeza uzito kupita kiasi,” amesema.Continue Reading