Rais Samia asimulia machungu mpunga wake ulivyoliwa na mifugo
Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan ameelezea machungu wanayokutana wakulima kwa mazao yao kuliwa na mifugo, huku akasimulia majibu ya dharau aliyopewa na mfugaji baada ya mifugo kula mpunga katika shamba lake, eneo la Dutumi, Mkoa wa Morogoro.
Akizungumza leo Julai 20, 2024 wakati akizungumza na machifu nchini, Rais Samia amesema kuna migogoro kati ya wakulima na wafugaji ambapo watu wamekuwa wakipigwa, kuuana na mazao yao kuliwa na mifugo.
“Niwaombe sana machifu wenzangu tukayasimamie haya. Tunapoacha wakulima na wafugaji wakauana na mara nyingi wanaoonewa ni wakulima, hii si haki. Nitakupeni mfano ulionipata mimi mwenyewe,” amesema.
Amesema aliwahi kulima mpunga katika eneo la Dutumi, Mkoa wa Morogoro na kwamba alilima mara ya kwanza kwa kuweka fedha yake yote kwenye shamba hilo.
“Basi wakaja watu na ng’ombe wao, mpunga umenawiri, nishasema hapa umasikini bye bye (kwa heri), dakika 10 nyingi mpunga wote ukaingia ng’ombe kama 300, wakaula. Sikuweza kufanya kitu chochote,” amesema.
Hata hivyo, amesema watoto wake walimweleza kuwa wajaribu tena kulima kwenye shamba hilo na hivyo akaamua kulima nusu ya eneo alilolima awali.
Amesema lakini mpunga ulivyoanza kuchanua na kuvutia na ukaanza kutoa harufu, ng’ombe waliingia tena katika shamba na kuula tena.
“Tulipokwenda katika kesi, mara hii nikasema hapana. Nikachukua mtendaji wa kijiji, polisi, sijui nani nikasema twende. Tulipokwenda katika kesi mfugaji anasema ng’ombe wangu kala mpunga wapi? Aliingia katika ghala ya nani, amekula majani tu,” amesema.
Rais Samia amesema inapotokea dharau ya namna hiyo ambayo inatolewa kwa mtu ambaye ameshapoteza nguvu na fedha na jasho, haileti amani Tanzania.
“Mfugaji anasema ng’ombe amekula majani tu, hajaingia katika ghala kula mpunga wa mtu. Sasa mambo kama haya yakitokea hayaleti amani Tanzania. Niwaombe sana machifu katika maeneo yetu tukayasimamie hayo,”amesema.
Aidha, Rais Samia amewataka Watanzania, viongozi wa Serikali, taasisi zisizo za kiserikali, viongozi wa kidini na machifu, kukemea vitendo viovu vinavyokiuka maadili ya Kitanzania.
“Tunapoona vitendo vya ovyo katika maeneo yetu, machifu tusemeni, tukemee. Kama mnamuona mkuu wenu wa wilaya hafanyi vyema mkemeeni, msemeni, muumbueni tumjue. Kama mnamuona kiongozi haendi mwendo mwema tuambieni tumjue ili tulete viongozi waadilifu na mambo yaende vizuri,” amesema.
Amesema mwongozo kwa ajili ya kuratibu shughuli za machifu nchini unaandaliwa, ambao ndio utaweka utaratibu wa kuwasema viongozi wanaokiuka maadili na sio kusimama na kuropoka.
“Niwaombe twende tukakemee vitendo viovu vinavyokiuka maadili yetu. Tudumishe upendo, amani, utu na kuheshimiana,” amesema.
Pia amewataka Watanzania wanapohama kutoka eneo moja kwenda jingine, kufuata mwongozo unaowataka kuchukua barua wanapotoka na kupeleka wanakokwenda ili kuwatambulisha.
“Lakini watu wanahamishana usiku na malori, wao na wanyama, wakifika mahali wanateremshana, pengine kuna mwenyeji anawasubiri wanavamia mapori, wanavamia misitu wanaingia huko,wengine wanafyeka mapori,” amesema.
Naye, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro amesema kwa sasa Serikali iko katika hatua za mwisho ya kuandaa mwongozo wa kutambua machifu na viongozi wa kimila, ili waweze kupata heshima wanayostahili kwa jamii na Serikali kwa ujumla.
“Mwongozo unaoandaliwa utatambua machifu na viongozi wa kimila katika ngazi ya wilaya na mikoa ili kutoa fursa kwa machifu kutekeleza jukumu lao la msingi la kuwawezesha Watanzania kuendelea kupata haki yao ya kikatiba na uhuru wa kuabudu kupitia mila, desturi na imani za kijadi,” amesema.
Aidha, Dk Ndumbaro amesema taarifa za uchumi za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mwaka 2023 zinaonyesha kuwa sekta ya utamaduni na sanaa inaongoza kwa kukua nchini ambapo imekuwa kwa asilimia 17.7.
Awali, Mwenyekiti wa Umoja wa machifu wa Tanzania, (UMT), Antonia Shangalai amesema kuwa Rais Samia amepandisha hadhi ya wanawake wa Tanzania kwa kuwapandisha vya kutosha na kuwataka mawaziri kutoa ushirikiano wa kutosha kwake.
“Sisi machifu tuko nyuma yenu tutaenzi mila, kuheshimiana, kuwaheshimu wakubwa na mambo yote yanayokwenda na mila na desturi zetu tusiyoyataka na nyie hamyataki na Serikali haiyataki. Tunaendelea kupambania hayo yasiendelee kuwepo kabisa,”amesema.
Akitoa baraka za machifu, Chifu Rocket Mwashinga amesema wakati nchi inaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, anahimiza Watanzania kulinda amani ya nchi na kuonya suala la ukabila.Continue Reading