Dk Biteko: Rais Samia kawapaisha wanawake sekta ya madini

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kufungua fursa za kuwawezesha wananchi kiuchumi ikiwa ni pamoja na kutilia mkazo ushirikishaji wa wanawake katika uchimbaji wa madini wenye tija.

Dk Biteko amesema hayo jijini Dar es Salaam juzi aliposhiriki kongamano maalumu kuelekea maadhimisho Siku ya Wanawake Duniani yanayoadhimishwa Machi 8, 2025.

Amesema kwa sasa kuna ongezeko kubwa la wanawake wanaoshiriki kwenye sekta ya madini ambayo kwa muda mrefu imeendelea kutawaliwa na wanaume.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, watu 6,030,575 wanajihusisha na shughuli mbalimbali za mnyororo wa thamani katika sekta ya madini na kati yao, wanawake ni 3,094,647 sawa na asilimia 51.3 ya watu wote wanaojihusisha na uchimbaji mdogo wa madini hususan katika sekta ndogo ya uziduaji.

Aidha, kati ya wachimbaji wadogo milioni 1.5, asilimia 27 kati yao wachimbaji hao ni wanawake.

“Katika kukuza ushiriki wa wanawake katika sekta hiyo, Rais Samia anasisitiza kutoa kipaumbele kwa wanawake kushiriki shughuli zote za kiuchumi kwa kuwapatia fursa za elimu na kumiliki rasilimali zilizopo kama kupata elimu, mikopo yenye masharti nafuu na kupata vifaa na vitendea kazi na kushiriki katika vikao mbalimbali vya maamuzi,” amesema Dk Biteko.

Amesema ushiriki wa wanawake katika sekta ya madini, ni msingi muhimu wa kukuza mnyororo wa thamani ndani ya jamii.

“Kutambua na kuthamini mchango wao, kunachangia maendeleo endelevu katika sekta hiyo,”amesema Dk Biteko.

Pia, amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kushiriki kikamilifu kupitia utekelezaji wa sera, sheria na taratibu mbalimbali.

Kupitia Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake (2023) na Sheria ya Madini (2017), pamoja na kanuni za ‘Local Content,’ Serikali inahakikisha wanawake wanapata fursa na rasilimali zinazowawezesha kushiriki kikamilifu sekta ya madini.

Amesema hatua za uwezeshaji wa kifedha na kitaaluma zinaendelea kutekelezwa kupitia taasisi za Serikali na wadau ikiwamo Kamisheni ya Madini Tanzania na Umoja wa Wachimba Madini Wanawake Tanzania (Tawoma).

Katika hafla hiyo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amewapongeza waandaaji wa mkutano huo kwa juhudi zao za kuendeleza ushiriki wa wanawake katika sekta ya uziduaji.

“Nimshukuru Rais Samia kwa juhudi zake za ushawishi wa kutaka mabadiliko ya Sheria ya Madini (2017), ambayo imeongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya madini,” amesema Mavunde.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis amesema maono ya Rais Samia ya kuunda taasisi inayoshughulikia masuala ya wanawake moja kwa moja ni hatua muhimu katika kuwawezesha wanawake, hasa wanaofanya kazi katika sekta ya madini.Continue Reading