Sheria mpya ya madini itakavyodhibiti utoroshaji madini, vito

Dar es Salaam. Baada ya mabadiliko ya sheria ya madini yaliyofanyika mwaka 2017, Serikali ya Tanzania imedhamiria kufanya mabadiliko mengine ili kuimarisha udhibiti wa matendo maovu katika sekta hiyo, ukiwemo utoroshaji madini.

Dhamira ya mabadiliko hayo ni kuhakikisha vitendo vya utoroshaji madini na vito vilivyokithiri katika migodi mbalimbali nchini vinadhibitiwa.

Akizungumzia hayo hivi karibuni, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amesema pamoja na mambo mengine, sheria hiyo inatarajiwa kumpa waziri mamlaka ya kuamua gharama za kodi na kwa kuanzia itakuwa asilimia 20 kwa kila anayezalisha madini.

“Kufanya hivi kutasaidia kutatua changamoto zilizopo kwenye masuala ya uchimbaji madini ambapo kuna kipengele kinawataka wachimbaji na wafanyabiashara kufuata taratibu za kisheria, lakini hawafanyi hivyo kwa madai ya utitiri wa kodi,” amesema.

Amesema Tanzania haipo tayari kuruhusu madini yake yatakatishwe katika mataifa mengine, akidokeza kufanya hivyo kunaiondolea nchi sifa yake.

“Kutokana na uaminifu ambao Tanzania imejiwekea, ni ngumu kutumia njia zisizofaa. Hivyo kutumia njia wanazotumia wengine ni kujiondolea sifa ya uaminifu ambayo tumejiwekea kimataifa,” amesema.

Mratibu Mkuu wa Miradi SwissAid, Alice Swai, amesema usafirishaji wa dhahabu usio na mfumo rasmi ndiyo chanzo cha kukosekana kwa taarifa za wachimbaji wadogo.

Kwa mujibu wa Swai, taarifa hizo hazijahusishwa katika ulinganisho wa taarifa za Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI), hivyo kuondolewa kwenye taarifa za kila mwaka za fedha.

“Kukosekana kwa taarifa za wachimbaji wadogo kumepelekea kuwepo na mianya ya kuruhusu usafirishaji wa dhahabu kwa mfumo usio rasmi,” amesema Alice.

Amesema kuna haja ya makubaliano ya nchi zinazopokea na kufanya biashara za madini kama uchakataji ili kuwa na mfumo wa pamoja kwa ajili ya kufuatilia taarifa za ugani katika mnyonyoro wa biashara ya kuuza na kununua madini.

“Kuna haja ya kupunguza mlolongo na kurahisisha mfumo wa kusafirisha madini nje ya nchi na kupunguza matamko, ili kukabiliana na usafirishwaji wa vipande vidogo vidogo kwa mtu binafsi kwa njia ya mabegi na ndege,” amesema.

Kwa mujibu wa Swai, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inapaswa itoe bei ya ushindani ili kuhamasisha wafanyabiashara licha ya kuwepo kwa muswada wa sheria ya fedha ya mwaka 2024, unaopunguza mrahaba kutoka asilimia sita hadi asilimia mbili na msamaha wa kibali cha kodi kwa asilimia moja.Continue Reading

Matobo kisheria yanavyochochea migogoro ya ardhi-3

Jana tuliona jinsi migogoro ya ardhi inavyoendelea kuongezeka nchini na tafiti zikitaja mipaka isiyoeleweka, ongezeko la watu na rushwa kama chanzo, huku Serikali ikieleza inayoyafanya. Leo tunaangazia athari za matobo yaliyomo kwenye sheria. Endelea…

Wakati migogoro ya ardhi iliyopokewa wizarani ikiongezeka mara sita zaidi mwaka 2023/2024 ikilinganishwa na mwaka 2021/2022, wataalamu wa sheria wanasema miongoni mwa sababu ni mkanganyiko na mianya iliyopo katika sheria zinazohusu ardhi.

Sheria zinazohusu ardhi nchini ni pamoja na; Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba Tano, Sura ya 114 iliyofanyiwa maboresho mwaka 2019, Sheria ya Ardhi Sura ya 113 ya mwaka 2002, Sheria ya Utwaaji Ardhi Sura ya 118, Sheria ya Usajili wa Ardhi Sura ya 334, na ile ya Mipango Miji Sheria namba 8 ya mwaka 2007.

Miongoni mwa ombwe lililoibuliwa ni sheria za ardhi nchini kujikita zaidi katika ardhi iliyosajiliwa kisheria na mara nyingi hazitoi mwongozo kamili kuhusu jinsi ya kuuza ardhi ambayo haijasajiliwa.

Moja ya sheria inayotajwa kuleta mkanganyiko na mwanya wa migogoro, kwa mujibu wa mwanasheria na mtafiti wa masuala ya kisheria, Luccian Lucelo ni Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba Tano, Sura ya 114 iliyofanyiwa maboresho mwaka 2019 ambayo inatoa mamlaka ya usimamizi wa ardhi kwa Serikali ya kijiji na haki ya umiliki (Customary right of occupancy) kupitia kifungu 20(1) cha sheria hiyo.

“Hii imekuwa miongoni mwa sheria ambazo zimekuwa na mianya, hasa kwenye utaratibu wa kuuza ardhi ambayo haijasajiliwa, tofauti na iliyosajiliwa kupitia Sheria ya Ardhi namba 4 Sura ya 113,” anasema Lucelo.

Mbali na hilo, Lucelo anatoa mfano wa kesi ya Kilango Semu Mjema vs Abdallah Mohamed Mnalindi (Land Appeal No. 8 of 2023) ukurasa wa 11 kuwa ilionyesha mwanya katika sheria hiyo.

“Sheria ya Ardhi Sura ya 114 haijatoa utaratibu wa uuzaji wa haki ya kutumia ardhi ya kijiji, badala yake wanatumia kifungu namba 10 cha Sheria za Mikataba, Sura ya 345.

“Pia Sheria ya Ardhi ya Kijiji Sura ya 114 haitoi moja kwa moja utaratibu wa uuzaji wa ardhi ambayo haijasajiliwa kupitia Sheria namba 5 ya Ardhi, badala yake sheria ipo kimya juu ya utaratibu sahihi wa uuzaji wa ardhi ambayo haijasajiliwa,” anasema Lucelo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Hakiardhi, Cathbert Tomitho anasema mkanganyiko mwingine katika sheria zinazosimamia ardhi ni kutoa mamlaka ya umiliki wa ardhi kwa Kamishna wa Ardhi na Serikali ya kijiji.

“Miongoni mwa mapungufu yaliyopo ni katika sheria ya ardhi ambayo inatoa mamlaka ya umiliki wa ardhi kwa Kamishna wa Ardhi kupitia kwa ofisa ardhi na Serikali ya mtaa, kwa hiyo unakuta kunakuwa na mkanganyiko.

“Mara kadhaa inatokea ardhi inauzwa na Serikali ya kijiji, lakini ukifika kwa ofisa ardhi kwa ajili ya taratibu nyingine, ikiwemo ya urasimishaji, kunakuwa na mkwamo kwa sababu sheria zimewapa nguvu wote,” anasema Tomitho ambaye pia ni mtafiti wa masuala ya ardhi.

Hoja ya Tomitho inarandana na Mwanasheria Kamanda Fundikira anayeyanyooshea kidole mabaraza ya ardhi ngazi ya kijiji na kata kufanya shughuli kinyume cha sheria kutokana na Sheria ya Ardhi ya Vijiji kuwapa mamlaka wanayoshindwa kuyatafsiri.

“Kumekuwa na changamoto sana katika sheria iliyoleta baraza la kata kwenye kutatua migogoro ya ardhi, kwani yamekuwa yakifanya uamuzi badala ya kupatanisha kama sheria inavyowataka,” anasema Fundikira.

Anasema kikwazo kingine ni sheria hiyo kuwapa nguvu katika masuala ya ardhi viongozi wa vijiji, lakini kutokana na kutokuzijua vyema wanavunja utaratibu hasa wa usawa wa kijinsia. Sheria inaelekeza kunatakiwa kuwe na usawa kati ya wanawake na wanaume.

Hoja ya wenyeviti wa vijiji wanaounda baraza la ardhi la kata kutofahamu sheria za ardhi na kusababisha baadhi ya migogoro ya rasilimali hiyo, pia imezungumzwa na Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji, Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Said Salehe anayesema wao wanajitahidi kutoa elimu.

“Katika eneo hili (wenyeviti wa vijiji) changamoto kweli ipo, na sisi (Mkuranga) tunajitahidi kufanya nao semina za mara kwa mara na kuwapitisha katika sheria, ili wayajue majukumu yao kwa usahihi,” anasema Salehe.

Miongoni mwa mapendekezo yanayotolewa kuziba mianya ya sheria hizi ni kufanyiwa marekebisho au kutungwa nyingine.

“Wadau tunaendelea kupigia kelele kurekebishwa sheria zote zenye mianya au kutunga sheria mpya zitakazoziba mianya iliyopo, ili tudhibiti ardhi isiuzwe kama nyanya sokoni. Hii ni rasilimali muhimu,” anasema Tomitho.

Kuhusu maboresho ya sheria, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dk Khatibu Kazungu alipotafutwa na Mwananchi kujua kama kuna marekebisho yoyote yaliyoletwa wizarani katika eneo hilo, aliomba watafutwe Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa maelezo zaidi.

“Samahani ni vyema ukiwatafuta Wizara ya Ardhi wanaweza kuwa na majibu mazuri zaidi, kwa sababu Tanzania ina sheria zaidi ya 400, hivyo wao wenyewe watakuwa wanajua kama kuna utaratibu unaoendelea,” anasema Kazungu.

Alipotafutwa, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda anasema mwingiliano wa baadhi ya majukumu katika sheria za ardhi si ombwe, bali ni miongoni mwa changamoto za kisheria na zitafanyiwa kazi.

“Hilo siyo ombwe, unajua sheria ni kama binadamu, unaanza kuwa mdogo na unakua na kuna mahitaji yanaongezeka. Sheria inafika mahali inazeeka na ikifika kipindi hicho hufanyiwa marekebisho au ikibidi kubadilishwa kabisa, vivyo hivyo inafanyika katika sheria za ardhi,” anasema Pinda.

Anasema kuna michakato mbalimbali (hakutaka kuiweka wazi) inaendelea kwa ajili ya kuziboresha sheria zinazosimamia ardhi nchini.

Hata hivyo, wakati wadau wengine wakilalamikia sheria hiyo kutoa mianya, Mhadhiri wa Sheria aliyebobea katika ardhi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Laurean Mussa anasema hauoni mkanganyiko wa kisheria katika migogoro ya ardhi.

Pia, anasema miongoni mwa suala linalopigiwa kelele la kuwahusisha viongozi wa Serikali za vijiji na mitaa katika ununuzi wa ardhi ni jema, kwani wao wanayafahamu zaidi maeneo yao.

“Sidhani kama kuna migogoro ya ardhi inayosababishwa na sheria, kwa sababu Serikali ya kijiji/mtaa kupitia kamati zao kazi yao ni kumshauri Kamishna wa Ardhi ambaye katika ngazi ya wilaya, ofisa ardhi ndiye anakasimiwa madaraka.

“Mwenyekiti wa kijiji kuhusika katika utambuzi na uuzaji wa ardhi ni suala jema kwa sababu yeye ndiye anayetambua eneo husika kwa ukubwa,” anasema.

Msimamo wa Waziri

Sakata la wenyeviti wa vijiji na mitaa si mara ya kwanza kuibuka, Desemba 22, 2023 katika kikao na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa alisema kazi ya uuzaji wa ardhi itafanywa na maofisa ardhi wa wilaya.

Pia, Waziri Silaa alitaka wananchi wasikubali kutoa asilimia 10 kuwapa viongozi hao (wa mitaa/vijiji) wanapofanya mauziano ya ardhi.

“Ili kuwa kwenye mipango miji wananchi epukeni kununua ardhi kwa wenyeviti wa vijiji na ikitokea unataka kununua, basi hakikisha unaitishwa mkutano wa kijiji na taratibu zote zinafuatwa, watakueleza masharti yao ikiwezekana chukua video ya huo mkutano siku mambo yakiharibika tuthibitishe,” alisema Silaa.

Nini kifanyike

Ili kupunguza mianya hiyo, Lucelo anapendekeza kufanyiwa marekebisho kwa sheria hizo na kutoa elimu ya kisheria miongoni mwa wananchi wanaouza na kununua ardhi.

“Sehemu yoyote yenye mwanya kisheria inatakiwa ifanyiwe kazi na kurekebishwa, pia elimu ya kisheria itolewe kuhusu haki na majukumu ya pande zinazoshiriki katika mauziano ya ardhi unaweza kusababisha kukosekana kwa makubaliano ya pamoja au uelewa sahihi, hivyo kuchochea migogoro kutokana na utaratibu kutoelezewa vizuri na sheria husika,” anasema.

“Upatikanaji wa njia za kisheria za kutatua migogoro ya ardhi uwe mkubwa, ili kuwe na mchakato mfupi katika kutatua migogoro,” anasema Lucelo.

Tomitho anatoa rai kwa wananchi kununua ardhi kwa kufuata sheria na si kiholela, ili kuepuka migogoro ya kisheria na mingine.

“Kila siku tunatoa elimu kwa wananchi, wasinunue ardhi kama nyanya au bidhaa nyingine, sheria zifuatwe ili kuepuka migogoro,” anasema Tomitho.

Itaendelea kesho, tutazungumzia talaka zinavyoathiri wanawake katika umiliki wa ardhi mkoani Pwani.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917Continue Reading

Kuonana na nabii mbinde, malipo yake mamilioni-2

Dar es Salaam. “Kama una Sh500,000 nenda pale kaandikishe jina lako uende kumuona nabii.”

Hii ni kauli ya mhudumu wa kanisa mojawapo la maombezi, akiwatangazia waumini, ikiwa ni sehemu ya kile ambacho Mwananchi limebaini katika mfululizo wa uchunguzi wake kuhusu waumini wa makanisa hayo wanavyokamuliwa mamilioni ya shilingi na viongozi wa dini ili waombewe au kubarikiwa.

Katika sehemu ya kwanza jana, tulibainisha jinsi baadhi ya makanisa jijini Dar es Salaam yanavyowafukarisha waumini kwa kuwatoza fedha nyingi kwa ununuzi wa maji, mafuta, au vitambaa, huku wengine wakilazimika kuuza mali zao.

Leo tunaangazia jinsi ilivyo vigumu na aghali kuwafikia manabii na mitume wa makanisa hayo, zikihitajika fedha nyingi kati ya Sh500,000 hadi Sh1.5 milioni na wakati mwingine hata zaidi ya hapo, huku ikielezwa kuwepo ushuhuda wa kuandaliwa ili kuuhadaa umma.

Katika moja ya makanisa ambayo Mwananchi limeyatembelea wilayani Temeke, ili uonane na kiongozi wa kanisa hilo, sharti utoe ada ya Sh500,000, bila kuhesabu sadaka nyingine wanazotozwa waumini.

Mchungaji huyo hurusha matangazo kwenye vyombo vya habari na mitandaoni kuhusu huduma zake, jambo ambalo limemvutia umati mkubwa wa waumini kusali kanisani hapo kila siku kuanzia Jumatatu hadi Jumapili.

Mwandishi wa Mwananchi alihudhuria baadhi ya ibada katika kanisa hilo, zikiwemo siku za Jumapili ambapo ibada huanza saa 1:00 asubuhi. Waumini hufika kanisani mapema asubuhi kusubiri uponyaji na unabii.

Kiongozi huyo mwenye walinzi wengi, aliingia kanisani saa 3 asubuhi akiwa kwenye msafara wa magari manne ya kifahari yaliyoandikwa jina lake.

Umati wa watu uliokuwa umefurika kanisani ulitoka kumlaki mtumishi huyo wa Mungu ambaye alishuka kutoka kwenye gari lake akiwa na walinzi sita. Moja kwa moja alielekea madhabahuni na kuanza ibada, ambapo baadhi ya waumini, hasa wanawake, walianza kupiga kelele na kugalagala wakidaiwa kuwa na mapepo na walitolewa nje.

Ndani ya ibada, mhudumu wa kanisa hilo alitangaza kuwa anayetaka kumuona mtumishi na kuombewa anatakiwa kutoa Sh500,000 ili atabiriwe na kupata uponyaji.

“Kama una Sh500,000 nenda pale kaandikishe jina lako uende kumuona nabii,” alisema msaidizi huyo.

Pia, alisema hadi saa nane mchana mtumishi alitangaza kila mtu awe amenunua maji yanayouzwa Sh2,000 ambayo yangeombewa, agizo ambalo waumini wengi walilitekeleza.

Kana kwamba haitoshi, waumini hao walitangaziwa kutoa sadaka yenye alama ya namba tatu, ikimaanisha Sh30,000, ambayo ilikuwa maalumu kwa ajili ya kufungua uchumi wa waumini hao.

Baada ya tangazo hilo, baadhi ya waumini walikimbilia bahasha zilizokuwa zikitolewa na mtumishi mwenyewe. Awamu iliyofuata, waliitwa wale kutoa Sh3,000, kima ambacho kilinyanyua wengi zaidi, na awamu ya mwisho ilihusisha kila mwenye kiasi chochote hata Sh100.

Baada ya kila mtu kutoa ‘alichonacho’, mtumishi huyo alitangaza ataonana na watu watatu tu waliotoa ada ya fomu ya Sh500, 000 na alifanya hivyo kwenye chumba maalumu baada ya kuhitimisha ibada.

Kutokana na umati mkubwa uliojaa karibu na chumba hicho, msaidizi wa mtumishi huyo alitoka na kutangaza kuwa wale tu walio na Sh500,000 ndio wangemuona mtumishi siku hiyo na kuwa wengine waliotoa pungufu wangeonana naye siku inayofuata.

Kila mtu aliyekuwa pale alijiandaa kuonana na mtumishi kwa viwango tofauti, wakidai Sh500, 000 ni nyingi. Wengine waliambatana na wagonjwa.

“Nipo hapa tangu jana nimelala hapa, tayari nimelipa Sh50,000 niliambiwa ningemuona leo, lakini leo naambiwa niongeze hela. Hii niliyotoa niliikopa na hapa nina nauli peke yake,” alisema Upendo Ngowi, mkazi wa Pwani, alipokuwa akiwabembeleza walinzi wa ‘mtumishi wa Mungu’.

Madai ya Upendo ni kuwa siku hiyo alikuwa amebakiwa na Sh10,000 za nauli ya kurudi nyumbani.

Jumapili aliambiwa aongeze fedha na arudi Jumatatu akiwa na walau Sh300,000, ili apate fomu ya kumuona mtumishi.

Hata hivyo, alishindwa na akawa anadai arejeshewe fedha zake akisema siku inayofuata asingeweza kuhudhuria ibada kwa kuwa anatokea mbali. Hata hivyo, fedha zake hazikurejeshwa.

Martha Urassa, mkazi wa Kimara ambaye anasumbuliwa na uvimbe kwenye titi, alisema amekuwa akihangaika kupata fursa ya maombi bila mafanikio.

“Niliambiwa nilipe hela ndio nionane na mtumishi, nimelipa Sh35,000 na bado sijamuona, naambiwa nikiwa na Sh500,000 ndio rahisi kumuona, huu umasikini ni mbaya sana,” alisema.

Kwa Suguye kwatajwa, afafanua

Katika Kanisa la The Word of Reconciliation Ministries (WRM), mmoja wa wahudumu ambaye hakutaka kutaja jina lake alieleza utaratibu wa kumuona Nabii Nicolaus Suguye katika siku za Jumatatu, Jumanne au Jumatano nako ni lazima uende na picha moja kwa ajili ya usajili, kisha mengine yatafuata.

Ukishaandikishwa na kusajiliwa, alisema pale utakapoonana na nabii huyo utatakiwa uwe na sadaka kuanzia Sh150,000 hadi Sh350,000 kwa ajili ya kuombewa.

“Wale waliosajiliwa kuna viti vyao kabisa kwa ajili ya kuonana ana kwa ana na Suguye na unapoonana naye lazima uwe na hela ya sadaka kuanzia Sh150,000 hadi Sh350,000 na ukishatoa fedha hizo utapatiwa mafuta, stika, maji na kitambaa,” alisema.

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari Machi 28, 2024 jijini Dar es Salaam kuhusu maadhimisho ya miaka 17 ya kanisa hilo, Suguye alikanusha kuwatoza fedha waumini wake.

“Hatutozi fedha katika kanisa kuombea watu, hata ukiwatafuta wanaokuja kujisajili mpaka sasa hakuna chochote na maombezi yangu ni bure na nayaendesha kwa kuwawekea mikono na baada ya hapo watu wanaondoka,” alifafanua Suguye baada ya kuulizwa.

Wakati Suguye akisema hayo, muumini wa kanisa hilo aliyejitambulisha kwa jina la Amina Salehe alidai yeye ana zaidi ya miaka mitatu anaabudu katika Kanisa la WRM na alitamani siku moja na yeye aguswe na nabii huyo lakini kutokana na kipato chake kuwa kidogo anashiriki kwenye ibada ya Jumapili pekee.

“Natamani na mimi nikutane na Nabii Suguye nifanyiwe maombi ya peke yangu, lakini kumuona ni gharama, kumuona kuanzia Sh150,000 na kuendelea, ila mimi nilienda kumuona nikiwa na Sh50,000, nilipofika kwa mtenda kazi (mhudumu) niliambiwa hela yangu ni ndogo,” alisema muumini huyo.

Wengine hadi mamilioni

Mwandishi wetu aliyepiga kambi katika kanisa mojawapo lililopo Kimara, Dar es Salaam, aliambiwa ili kuonana na kiongozi wa kanisa hilo sharti alipe Sh1.5 milioni.

Mwandishi aliambiwa ajaze fomu inayoitwa jina ‘nguzo ya ujenzi’ ambayo alitakiwa kuilipia Sh1.5 milioni.

“Ukitoa hiyo sadaka, unamuona mapema sana, lakini hivihivi, itakulazimu usubiri foleni na ni kubwa mno,” alisema mtendaji ambaye jina lake limehifadhiwa.

Akifafanua zaidi, mtenda kazi huyo alisema: “Kadi ya nguzo ni Sh1.5 milioni ambayo ukimaliza kuilipia inagongwa muhuri na baba mwenyewe (anamtaja jina) kisha unapewa nafasi ya kwenda kuonana naye moja kwa moja ofisini kwake, unamweleza matatizo yako,” alisema.

Alisema kadi hizo anazitoa mwenyewe (nabii) pale madhabahuni na zinaweza kulipiwa kidogo kidogo hadi mtu amalize.

“Ukimaliza kuilipia Kadi ya Nguzo hausubiri foleni, hiyo ni ‘fasta’ tu, gharama ya awali ya kuipata hiyo kadi ni Sh10, 000, kama unailipia kidogo kidogo, kila unapolipa sadaka yako inaandikwa hadi ukimaliza baba mwenyewe anaigonga muhuri, unapata kibali cha kwenda kumuona moja kwa moja,” alisema.

Ushuhuda wa kupanga

Katika uchunguzi wa makanisa hayo kumebainika udanganyifu na uwepo miujiza ya uongo inayoenea kwa kasi nchini Tanzania, ambapo watu binafsi wanatumiwa kutunga miujiza na ushuhuda kwa lengo la kuuaminisha umma.

Hii inahusisha kundi la watu, mara nyingi kutoka nje ya nchi, wanaodai kuteseka na maradhi sugu kama saratani na kisukari.

Uchunguzi umebaini kuwa baadhi yao wana ulemavu bandia kama wa kutokusikia na upofu.

Timoth (si jina halisi), mshiriki wa zamani kwenye moja ya makanisa, anaeleza kuwa huwa wanatoka nje ya eneo la ibada ili kuepuka kutambuliwa na kueleza tatizo fulani.

Baada ya miezi kadhaa, wanarudi wakidai wameponywa kimiujiza, jambo linaloshawishi wafuasi kuweka imani na fedha zao katika madhabahu hizo. Timoth anasema wachungaji huweka mazingira waumini kushindwa kufikiri kwa makini na kuwataka wajitenge na wapinzani.

Hata Beatrice (pia si jina halisi) anaeleza wameandaliwa kujifanya wameponywa wakati wa ibada na kupiga simu kupitia redio ay TV ambapo ‘mtu wa Mungu’ anatoa unabii.

Hali hii nchini inatia wasiwasi, ingawa haijafikia viwango vya Kenya na Afrika Kusini. Wachungaji hufikia hatua ya kutumia nguvu zisizo za kawaida kutoka Nigeria ili kuwavuta waumini.

Itaendelea toleo lijalo, tukiangazia vifaa mbalimbali wanavyonunua waumini ka uponyaji na miujiza.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.Continue Reading

Wataalamu wapendekeza udhibiti bidhaa za mafuta Tanzania

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya nchini Tanzania wamependekeza udhibiti wa uingizwaji wa mafuta na bidhaa zake, kama mbinu ya kuepuka magojwa yasiyo ya kuambukiza kwa wananchi.

Mafuta waliyopendekeza yadhibitiwe ni yale yasiyoandaliwa vizuri na yenye hatari kubwa kwa matumizi ya binadamu.

Sambamba na hilo, wataalamu hao wamesema kama inawezekana itafutwe namna ya kuongezwa kodi kwa aina hiyo ya mafuta, wakati yale yaliyo salama yapunguziwe kodi.

Wataalamu hao wamesema hayo leo, Jumatatu Julai 8, 2024 walipokuwa wakichangia kwenye mjadala wa Mwananchi Space, uliojadili ‘Ulaji wa vyakula vya mafuta mengi na athari zake ulioandaliwa kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC).

Ofisa Lishe na Mtafiti Mwandamizi TFNC, Maria Ngillisho amesema vyakula vinavyopikwa kwa mafuta mengi vinavutia na vitamu, lakini vina madhara makubwa mwilini.

Amesema kupika kwa mafuta ni njia rahisi, lakini ina athari kiafya hasa vyakula hivyo vikitumiwa kwa wingi na mara kwa mara.

“Tuna vyakula tunavyopika kwenye mafuta mengi na hivi tunaweza kuviepuka kwa kupika kwa kutumia mbinu nyingine ikiwemo kuoka,” amesema.

Maria ameeleza vyakula vyenye mafuta mengi ni vile vyenye asili ya mafuta na vinavyopikwa kwa mafuta mengi.

Amevitaja vyakula hivyo ni karanga, mbegu za alizeti, korosho na vile vyenye asili ya mimea.

Naye Mkuu wa kitengo cha Utafiti na daktari bingwa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Pedro Pallangyo amesema kiwango kikubwa cha mafuta kinasababisha mwili ushindwe kuyatumia katika shughuli za kawaida.

Hatua hiyo, amesema inasababisha yajihifadhiwe sehemu mbalimbali na hivyo kusababisha magonjwa.

“Dalili ya kuakisi kuwa mafuta ni namna anavyoongezeka uzito, kiribatumbo na mabadiliko hayo yanakuwa ndani ya mili yetu, hasa mafuta yanapoingia katika mfumo wa moyo na mishipa ya damu,” amesema.

Amesema binadamu walivyoumbwa mili yao ina mishipa ya damu yenye upenyo mdogo ambao damu inapita na ukubwa wake ni sahihi katika kukidhi mahitaji.

“Mafuta yakitanda katika mishipa mikubwa ya damu ukubwa wake unapungua, sasa inategemeana imetanda katika mishipa ipi ina maana hayo maeneo yatapokea kiwango kidogo cha damu kuliko inavyotakiwa,” amesema.

Amesema kutokana na wimbi la mafuta katika jamii hata vijana wanaanza kuonekana na magojwa hayo, huku akieleza wengi wanakuja na malalamiko ya magonjwa ya miguu na kuanza kubadilika rangi.

“Tafsiri ya haraka maeneo yaliyobadilika rangi hayapati kiwango cha damu ya kutosha na ukifanya uchunguzi wa miguu ya hao wahusika unaona mishipa midogo midogo inayolisha miguu inakuwa imeziba,” amesema.

Amesema kumekuwa na ongezeko la watu wengi kuziba mishipa mitatu ya moyo inayosababisha vifo vya ghafla kwa kuwa wanakosa hewa ya oskjeni kwenye moyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza wa Wizara ya Afya, Dk Omary Ubuguyu amesema kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, kwa mwaka Serikali huitaji Sh1.1 trilioni kukabiliana na magonjwa hayo.

“Sisi tukiangalia mkakati wetu wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza tunahitaji Sh1.1 trilioni kwa mwaka kutoa huduma stahiki kutoa huduma stahiki kwa magonjwa sawa na bajeti nzima ya Wizara ya Afya inayotolewa sasa,” amesema Dk Ubuguyu.

Dk Ubuguyu amesema nchi imefika katika kiwango cha ukubwa wa tatizo kwa sababu walichelewa kuanza kupambana na magonjwa hayo, kwani waliamini ni tatizo linalowapata zaidi watu wa ukanda wa Afrika Magharibi.

Naye Mtaalamu wa lishe wa TFNC, Elizabeth Lyimo amesema mafuta ni moja ya kundi la chakula lenye kazi maalumu mwilini kutokana na virutubisho vilivyopo.

“Kundi hili linapaswa liliwe kwa kuangaliwa kwa sababu linatoa kiwango kikubwa cha nishati lishe, laikini kuna aina mbili za mafuta ya kimiminika (yasiyo ganda) ni yale yanayotokana na mimea na yanayoganda yanatokana na wanayama,” amesema.

Awali, Mhariri wa Jarida la Afya Gazeti la Mwananchi, Herieth Makwetta akichokoza mada amesema ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi ni chanzo cha magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwemo shinikizo la damu na saratani.

“Utafiti wa mwisho uliofanywa na Wizara ya Afya mwaka 2018 unaonyesha asilimia 33 ya vifo vyote vilivyotokea nchini vilisababishwa na magonjwa yasiyoambukizwa,” amesema.

Katika maelezo yake Makwetta, amefafanua wataalamu wanaonya kuwa ifikapo mwaka 2027, huenda vifo vinavyotokana na hayo magonjwa vitafikilia asilimia 54.

“Wataalamu wanasema mafuta yanahitaji kiwango kidogo mwilini kwa kazi ya kumpatia nguvu kiasi cha dole gumba, lakini wengi wamekuwa wakikiuka na kujikuta wakiongeza uzito kupita kiasi,” amesema.Continue Reading

Sabasaba yamkumbusha Kikwete enzi za utawala wake

Dar es Salaam. Rais mstaafu Jakaya Kikwete amesema Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DIFT) yamekuwa ya kipekee kwa kuboreshwa miundombinu, hususani ya barabara tofauti na miaka ya nyuma.

Kikwete ameeleza hayo leo Julai 6, 2024 alipotembelea maonyesho hayo maarufu Sabasaba.

Katika mazungumzo yake alikuwa akilinganisha hali anayoiona na miaka ya nyuma, hususani wakati wa utawala wake.

“Kipindi changu wakati nakuja barabara zilikuwa za vumbi na maombi yangu yalikuwa ni kuhakikisha barabara zinawekwa lami maana ilikuwa unakuja huna mafua lakini unaondoka na mafua,” amesema.

Pia amesema alikuwa anaangalia uboreshaji wa mabanda na bidhaa zinazoonyeshwa kuanzia kwa wageni hadi wazawa na hata waelekezaji wamekuwa wakieleza kitu kwa ufasaha tofauti na miaka ya nyuma.

Akizungumzia nishati safi, Kikwete amesema wakati anapokea uongozi matumizi ya umeme yalikuwa asilimia 10 na matumizi makubwa yalikuwa mjini na siyo kijiji.

Amesema waliamua kuanzisha mradi wa umeme vijijini ambao ulianzia kwa hayati Rais Benjamin Mkapa na yeye alilikamilisha na alipokwenda kwenye ziara mkoani Mara alizindua umeme vijijini na wakati huo ukiwa kwenye vijiji 206.

Wakati huo watu walikuwa wanahitaji umeme vijijini na wangeachiwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambao wanafanya biashara wao wanaangalia sehemu ambayo walikuwa na uhakika wa biashara.

Kikwete ametoa wito kwa watoa huduma wa umeme na gesi kuangalia bei wanazotoza zisiwaumize watumiaji kwani inaweza kuwa sababu ya kurudi kwenye matumizi ya mkaa na kuni.

“Sijui kama takwimu zimebadilika Dar es Salaam walikuwa wanatumia magunia ya mkaa 40,000 kwa siku ni kwa kiasi gani miti imepotea hapo,” amehoji.

Kikwete ametumia zaidi ya saa tano kuzunguka viwanja vya maonyesho vya Mwalimu Julius Nyerere vilivyopo Barabara ya Kilwa.

Aliingia uwanjani saa 5.30 asubuhi na hadi saa 11.00 jioni alikuwa bado akizunguka kwenye mabanda kuangalia bidhaa, kununua na kuacha maoni katika baadhi ya sehemu alizotembelea.Continue Reading

RC Mtanda aipa mbinu ATCL kuhimili soko la ushindani

Mwanza. Wakati Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) likitarajia kupokea ndege mpya aina ya Boeing 787- 800 Dreamliner, shirika hilo limeshauriwa kuboresha huduma kwa wateja na kuongeza idadi ya safari ili kuvutia wateja na kustahimili kwenye soko la usafirishaji wa anga nchini.

Wito huo umetolewa leo Jumatano Julai 3, 2024, na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jengo maalum la wateja wa hadhi ya juu ‘Business Class’ lililojengwa na Shirika la VIA Aviation katika Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Mwanza.

Huku akidokeza ofisi yake ofa nane za kampuni za ndege za kimataifa kuhitaji kufanya safari katika uwanja huo, Mtanda ameeleza kutofurahishwa na tabia ya safari za ndege za shirika hilo kuahirishwa bila wateja kujulishwa jambo alilodai ni kufanya kazi kwa mazoea na kusababisha usumbufu kwa wateja.

“Ninayasema haya kwa sababu hii ni biashara na tusipozungumza wakati wateja wenu wanalalamika kwenye suala hilo tutakuwa hatutendi haki. Ili muweze kushindana na wengine lazima muboreshe huduma kwa wateja kwa sababu biashara ni ushindani na huduma kwa wateja,” amesema Mtanda.

Kupitia mkoa huo wenye wakazi zaidi ya milioni 3.6 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022, Mtanda amesema wageni na wenyeji wake wanategema huduma ya usafiri wa anga huku kimbilio lao likiwa ni ATCL. Pia ameiomba ATCL kuweka unafuu wa gharama ya nauli ili kumwezesha kila mwananchi kutumia huduma zake.

“Hapa Mwanza ili upate tiketi ya Air Tanzania lazima uikate siku tatu, nne au tano kabla ya safari ndani ya siku mbili kuelekea safari yako huwezi kupata tiketi maana yake watu wenye haraka na wenye dharura hawawezi kusafiri,” amesema.

“Hata mimi RC nikiitwa Dar es Salaam inabidi nibanane na meneja nimwambie nimeitwa pale Ikulu sasa atalazimika atafute abiria mwenye unyenyekevu ampunguze kwa sababu Serikali lazima iwe kazini muda wote. Matindi ututafutie ndege nyingine ikibidi hiyo inayokuja ileteni Mwanza,” amesema Mtanda.

Kiongozi huyo amesema katika kutambua changamoto ya usafiri wa anga mkoani Mwanza, Serikali inatumia Sh13 bilioni kufanya maboresho katika jengo la abiria ambalo likikamilika litahudumia abiria wa kitaifa zaidi ya 800 na kimataifa zaidi ya 600 kwa wakati mmoja.

“Yale mambo ya ku-cancel (kuahirisha safari za ndege) halafu tunakuja hadi uwanjani hata meseji hakuna, Matindi hilo lifanyieni kazi. Siku moja nakuja hapa naambiwa eti hiyo ndege imeahirisha safari leo sasa simu zetu si hawa watu wa ATCL wanazo. Wananyue simu watuarifu,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu ATCL, Ladislaus Matindi amekiri mahitaji ya Mkoa wa Mwanza kwa huduma hiyo kuwa makubwa huku akidokeza kuwa shirika hilo lazima lihakikishe huduma hiyo inafikishwa kila eneo nchini ili kufikisha huduma kwa kila mtanzania bila kujali mahala alipo.

“Ndege kubwa inakuja asubuhi na jioni, mchana zinakuja hizo ndege ndogo bado hazitoshelezi mahitaji ya wenzetu wa Mwanza, ndani ya nchi tunakwenda vituo 10 ikiwemo Kilimajaro, Bukoba, Songea, Mbeya, Arusha, Kigoma, Zanzibar wote hawa lazima wapate huduma ili ni shirika la Watanzania lazima wahudumiwe wote hata kwa kiasi kidogo,” amesema Matindi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Biashara na Mauzo wa ATCL, Patrick Ndekana hadi kufikia Juni 2024, ATCL imebeba abiria 1,123,696, wastani wa abiria 93,000 kwa mwezi huku abiria 253,593 kati yao wakibebwa kutoka na kwenda kituo cha Mwanza pekee sawa na asilimia 23 ya abiria wote waliobebwa katika safari za shirika hilo.

“Wastani wa ujazo ni zaidi ya similia 90 hii ikiashirika kuna uhitaji wa kuongeza miruko kwa mkoa wa Mwanza. Kuanzia Julai 14, 2024, tutaanza kutumia ndege aina ya Boeing 737 Max 9 yenye uwezo wa kubeba abiria 181 kwa tripu moja na tani mbili za mizigo. Hii itakuwa chachu itatuwezesha kutoa huduma ya usafiri wa anga nchini na mizigo, hii ni ongezeko la viti takribani 49,” amesema Ndekana.

Ndekana amesema kwa sasa ndege kubwa inayofanya safari zake kwenda Mwanza ni Airbus 220 inayobeba abiria 132, hivyo, kuongeza uwezo wa abiria 49 kutaongeza ufanisi na huduma kwa wakazi wa mkoa huo.

“ATCL ina ndege 14 zinazoruka na tunategemea kupokea ndege moja aina ya Boeng 787-800 mwezi Agosti. Pia tuna ndege ndogo ya viti 50 ambayo ni Bombadier Q300 ambayo tunategema ilikuwa matengezo muda wowote kuanzia sasa itakuwa kwenye operesheni zetu,” amesema Ndekana.

Katika hatua nyingine, Ndekana amesema uzinduzi wa jengo hilo maarufu kama ‘Serengeti Lounge Via Aviation’ litasaidia kuboresha huduma kwa wateja wa waaminifu wa ATCL zaidi ya 58, 475, wateja 870 kati yao wakiwa wa daraja la juu. Pia amesema Novemba mwaka huu, shirika hilo litaongeza safari za ndege kwenda Dubai kutoa nne kwa wiki hadi kila siku.Continue Reading