Ushuru kwenye ‘tomato sauce’ wapingwa

Dar es Salaam. Hatua ya Serikali kupendekeza kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha Sh300 kwa kilo ya tomato sauce na tomato ketchup, chilli sauce na chilli ketchup zinazotoka nje ya nchi, imeelezwa na wadau wa uchumi kuwa inatokana na kukosekana ubunifu wa vyanzo vya mapato.

Akiwasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25 bungeni Juni 13, 2024, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alisema lengo la hatua hiyo ni kuongeza mapato ya Serikali na kupata fedha za fidia ya athari hasi zinazotokana na matumizi ya sukari na chumvi iliyopo katika bidhaa hizo, hatua ambayo alisema inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh634 milioni.

Baadhi ya wachumi na wataalamu wa lishe waliozungumza na Mwananchi Juni 15, 2024 wamesema kama Serikali imekusudia kudhibiti matumizi ya bidhaa hizo haipaswi kuzungumzia suala la makusanyo.

Wamehoji ni kwa namna gani mtu aliyeathiriwa na bidhaa hizo anapatiwa fidia.

Dk Godfrey Malisa, mchambuzi wa masuala ya siasa na uchumi, amesema ushuru unaopendekezwa ni kutokana na bajeti kuwa tegemezi kwa kiasi kikubwa, akisisitiza Tanzania ina vyanzo vingi vya mapato lakini hakuna ubunifu wa kupata vipya badala yake vitu vidogo ambavyo tayari vina kodi vinaenda kuongezewa mzigo.

“Zipo nyingi zina athari na hazijaguswa, ukisema unaweka kodi hizi kwa sababu hiyo, ukiingia sokoni zipo bidhaa zina athari kubwa kuliko hizo na hazijaguswa, ukiongeza hizo hela ndiyo suluhu ya kupunguza athari?”amehoji Dk Malisa.

Amesema wananchi wa kawaida hivi sasa wamekatishwa tamaa kulipa kodi kwa hiari kutokana na matumizi yake kutoendana na mahitaji yao.

Profesa Haji Semboja, mwanataaluma ya uchumi amesema nchi yoyote, kutokana na sera zake, inaweza kuweka mbinu ya kutekeleza sera kutokana na sababu za kimaisha, mazingira, kisiasa na kiuchumi.

“Kuongeza ushuru kwenye bidhaa maana yake hutaki mtu huyo atumie kitu hicho kutokana na sababu za kiafya, mfano sigara na vilevi na hii inaweza kutekelezwa kupitia sera za nchi au nje ya nchi, tatizo ni kwamba ukisema unatekeleza hilo kupata fedha si sahihi, ulipaswa tuishie kuzuia athari,” amesema.

Amesema uwekaji wa ushuru kwenye bidhaa hizo iwe ni kwa sababu za kiafya pekee na si kuongeza mapato.

Mtaalamu wa lishe, Emmanuel Maganga amesema kuweka ushuru kwa bidhaa zinazotoka nje kwa lengo la kufidia athari kiafya, haina maana.

“Kwa hiyo fidia mtu aliyeathirika anasaidiwaje? Sioni kama ina mantiki kwa sababu tayari umeruhusu na watu wanaathirika na unapokea fidia hiyo, ina maana gani?” amehoji.

Hata hivyo, mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la Chakula la Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Stella Kimambo amesema kiafya matumizi ya vyakula vilivyosindikwa viwandani si salama kwa afya.

Amesema hatua ya kuwekwa ushuru ni moja ya mikakati ya kuwasaidia wananchi kuondokana na matumizi ya bidhaa hizo ambazo zimekuwa na mchango mkubwa wa maradhi yasiyo ya kuambukiza kama kisukari, maradhi ya moyo na kiharusi.

“Hata nchi zingine zinapoona chakula kina madhara, zinaweza kuongeza ushuru. Tuna nyanya nyingi na zinapotea kutokana na kutokuwa na viwanda, hatua hizi za kutoza ushuru bidhaa za nje ni sehemu ya kuimarisha soko la ndani,” amesema.

Akizungumzia madhara ya chumvi, mtaalamu wa lishe, Fatma Mwasora amesema japo bidhaa hiyo ina umuhimu mwilini, matumizi yake yanapaswa kuwa madogo.

“Watu wenye matatizo ya maradhi ya kudumu wanapaswa kupata ushauri kwa daktari,” amesema.

Miongoni mwa hatari za matumizi ya chumvi na sukari ni kuchangia shinikizo la juu la damu, kisukari, moyo, kiharusi na saratani, magonjwa ambayo kwa mujibu wa Wizara ya Afya, bajeti ya kuhudumia magonjwa yasiyoambukiza iliongezeka mara tatu mwaka 2021/22 hadi kufikia Sh99.08 bilioni ukilinganisha na Sh35.65 bilioni mwaka 2016/17.

Takwimu zinaonyesha shinikizo la juu la damu lipo kati ya asilimia 20 hadi 30 ikiwa na maana kuwa katika kila wananchi 10, wawili hadi watatu wana tatizo hilo.

Uhalisia ulivyo

Kwa mujibu wa tovuti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kiwango cha chumvi ambacho ni salama kinachopendekezwa kutumika kwa siku ni miligramu 1,500 takribani nusu kijiko cha chai na isizidi miligramu 2,000.

Bidhaa ya tomato Ketchup kwa mujibu wa Taasisi ya Moyo ya British Heart Foundation ya nchini Uingereza, kuna gramu 0.3 za chumvi na gramu 4.1 ya sukari kwenye kijiko kikubwa cha chakula cha bidhaa hiyo.Continue Reading

Afrika yakabiliwa na uhaba wa marubani,wahandisi

Arusha. Ushindani katika usafiri wa anga katika Bara la Afrika unatajwa kuwa mdogo kutokana na mashirika ya ndege kuwa machache na kuwa yakiongezeka yatasaidia kuongeza ushindani,nauli kushuka pamoja na ubora wa huduma kuongezeka.

Aidha, bara hilo linatajwa kuwa na upungufu wa rasilimali watu wakiwemo marubani na wahandisi katika sekta hiyo muhimu ambayo inazidi kukua kwa kasi.

Kutokana na sababu hizo, wakurugenzi wakuu na wakuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Afrika ( AFCAC), wanakutana jijini Arusha kwa siku mbili kujadili namna ya kuboresha sekta hiyo.

Akizungumza katika mkutano huo leo Jumatano Juni 5, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa anga nchini (TCAA), Hamza Johari, amesema malengo makubwa ni kuweka mikakati ya pamoja katika bara hilo kuhakikisha usafiri wa anga unakuwa salama.

“Tunataka tuangalie masuala ya kiushindani katika usafiri wa anga,tumeona kwamba ushindani si mkubwa sana kwani mashirika ya ndege ni machache,yanapokuwa machache nauli nazo zinakuwa juu tunataka yawe mengi,yanavyokuwa mengi yakashindana vizuri basi nauli na zenyewe zitarekebika.

” Tunataka tuangalie masuala ya rasilimali watu kwa maana ya kwamba tuna upungufu wa idadi ya marubani wanaohitajika katika sekta upungufu wa wahandisi wanaohitajika pia,”amesema Johari.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa Oktoba 5, 2023 mkurugenzi huyo, amesema kuanzia mwaka 2003 hadi 2023, idadi ya ndege zilizokuwa zinatoa huduma katika anga la Tanzania zimeongezeka kutoka 101 hadi 206,marubani wakitoka 234 hadi 603 huku waongoza ndege wakiongezeka kutoka 70 hadi kufikia 154.

Amesema kulikuwa na ongezeko la wakaguzi wa usalama kutoka 28 hadi 44, wahandisi wa mitambo ya viwanja wakiongezeka kutoka 20 hadi 44 na wataalam wa anga wakiongezeka kutoka 50 hadi kufika 83.

Kuhusu marubani amesema Tanzania inahitaji marubani 780 hivyo kuna upungufu mkubwa kuendana na kasi ya ukuaji ambapo hadi wakati huo walifadhili marubani 22 waliokuwa wakisoma nje ya nchi ila kwa sasa NIT itafundisha kwa Dola 48,000 ambazo ni sawa na Sh120.3 milioni badala ya Dola 120,000 zilizokiwa sawa na Sh300.9 milioni.

Hatua nyingine ni kuhakikisha usafiri wa anga Afrika unazidi kuwa salama na endelevu na kuwa wataangalia eneo la ulinzi kwani kumekuwa na tabia ya watu wenye nia ovu ikiwemo magaidi,kuteka ndege, kulipua viwanja na kutega mabomu japo matukio hayo hayatokei kwa wingi katika bara la Afrika lakini lazima wachukue tahadhari.

“Sasa hivi dunia imekua katika teknolojia kila kitu kinakwenda kidijitali na tunavyokwenda kwenye ulimwengu huo kunaweza kutokea mashambulio ya mifumo na mifumo ikiharibika tutashindwa kufanya shughuli zetu,tutaangalia zaidi uhalifu huo wa mitandaoni ili tusije kushambuliwa na tutengeneze sauti moja kama Afrika,”ameongeza Johari.

Akifungua mkutano huo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema wakuu hao watajadiliana na kutoka na maazimio ya pamoja katika kuboresha usafiri huo pamoja na miundombinu huku suala la usalama likipewa kipaumbele kwani bila usalama hakuna usafiri wa anga wa uhakika.

Kuhusu suala la uchafuzi wa mazingira,Waziri Mbarawa amesema wakuu hao na wataalamu wa sekta ya anga watajadiliana jinsi wanaweza kuhakikisha anga linakuwa safi na salama na kuongeza maendeleo katika nchi hizo.

“Tanzania tumefanya kazi kubwa kwenye sekta ya usafiri wa anga na tuna miradi mbalimbali inaendelea na lengo la Serikali ni kuendelea kufungua usafiri wa anga na kuifanya anga zetu ziwe salama.

“Tunaendelea na ujenzi mkubwa wa viwanja vya ndege katika mikoa mbalimbali ikiwemo kiwanja cha Msalato Dodoma ambacho kitagharimu zaidi ya Sh365 bilioni,”amesema.

Waziri huyo amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha mikoa yote inakuwa na viwanja vya ndege vya kisasa na kuwataka Watanzania waendelee kutumia usafiri huo ambao ni usalama zaidi ukilinganisha na usafiri mwingine.Continue Reading