Bomba la Tazama kupanuliwa, Tanzania, Zambia wajadiliana

Bomba la Tazama kupanuliwa, Tanzania, Zambia wajadiliana

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na ile ya Zambia zipo katika mazungumzo yanayolenga kuongeza uwekezaji katika bomba la Mafuta la Tanzania – Zambia (TAZAMA).

Mazungumzo hayo yanalenga kupanua bomba la mafuta kutoka inchi 8 hadi inchi 12 ili kuliwezesha kuwa na uwezo wa kusafirisha mafuta mengi zaidi kwenda nchini Zambia na nchi nyingine za jirani.

Mbali na hilo, pia zipo katika mkakati wa kujenga bomba jipya litakalokuwa na inchi 24 ili kuongeza usafirishaji.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu, Agosti 26, 2024 wakati Serikali ikipokea gawio la Sh4.35 bilioni kutoka Tazama Pipeline ikiwa ni sehemu ya faida waliyotengeneza.

Akizungumza baada ya kupokea gawio hilo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema lengo la kufanya uwekezaji huo sasa ni kushusha gharama kwa wamiliki wa vituo vya mafuta katika maeneo ambayo bomba linapita.

“Mbali na upanuzi pia tunatarajia kuanza ujenzi wa bomba jipya la inchI 24 na hili lipo katika hatua za ununuzi kabla utekelezaji haujaanza,” amesema Dk Biteko.

Amesema lengo ni kuona utumiaji wa malori katika kusafirisha mafuta unapungua na watu wengi wanahamia katika kutumia bomba kwa kuchukua mafuta katika baadhi ya vituo vitakavyowekwa katika mikoa husika.

“Lengo letu ni mafuta yanayokwenda mikoa ya kusini kwa kutumia malori,  yasafirishwe kwa bomba,” amesema Dk Biteko.

Amesema kufanya hivyo kunalenga kuhakikisha Watanzania wanapata mafuta kwa bei nafuu kwa sababu gharama za usafirishaji, ni miongoni mwa vitu vinavyochangia kuongezeka kwa bei ya mafuta ya rejareja.

Pia, kufanya hivyo kutasaidia kulinda barabara zisiharibike haraka kutokana na usafirishaji unaofanywa kwa kutumia malori.

Akizungumzia gawio hilo, Dk Biteko amesema ni moja ya hatua njema ambayo inatia moyo. Amesema Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara nchini Zambia moja ya maelekezo aliyotoa ni kuhakikisha miradi inayotekelezwa na nchi hizo mbili ina inasimamiwa ili kuleta manufaa.

“Pia miradi hii ichangie katika kubadilisha maisha ya watu na hali zao na kwa sababu tulikuwa hatujapata gawio tangu mwaka 2019, niliwaita nikawauliza wakasema wataleta hela na leo wameleta,” amesema Dk Biteko.

Akifafanua kuhusu ujenzi wa bomba jipya, Mkurugenzi Mtendaji wa Tazama, Davison Thawethe amesema bomba hilo jipya litakuwa na uwezo wa kusafirisha futi za ujazi milioni tano za mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Ndola Zambia kwa mwaka.

“Tumeagiza kampuni kufanya upembuzi yakinifu utakaoanza siku yoyote kuanzia sasa ili kubaini bomba hilo litagharimu kiasi gani,” amesema.

Amesema uamuzi wa kujenga bomba jipya ni kuendana na ukuaji wa bidhaa za mafuta unaoongezeka kila mwaka.

Awali, Mwenyekiti wa bodi wa kampuni hiyo, Peter Mumba amesema gawio hilo limetokana na utendaji mzuri walioushuhudia licha ya baadhi ya changamoto walizopitia.

“Jambo hilo limefanya kuboresha utoaji wetu wa huduma, jitihada hizi hazijaimarisha uhudumiaji wateja tu bali pia uwezo wetu wa kifedha,” amesema Mumba.

Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema shirika la Tazama lilianza miaka 58 iliyopita na kama ingekuwa ni umri wa mtu basi amebakiza miaka miwili kabla hajastaafu.

Amesema kipindi hicho mtu huwa ameishiwa nguvu ila ni tofauti na Tazama ambao umri huo ndiyo wanaanza kuamka na kupata nguvu kubwa.

Amesema fedha hizo zitakwenda kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama ilivyoelekezwa.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories

High Court rejects Transworld’s application
Tanzania Foreign Investment News
Investment News Editor

High Court rejects Transworld’s application

The High Court in Dar es Salaam has struck out an application in which Transworld Aviation, a ground handler at the Abeid Aman Karume International Airport (AAKIA) was seeking permission to sue the Tanzania Civil Aviation Authority (TCAA).Continue Reading