Dar es Salaam. Tanzania na Uturuki zimekubaliana kukuza biashara ya pamoja hadi kufikia Sh2.58 trilioni kutoka Sh890 bilioni iliyopo sasa.
Wakati azma hiyo ikiwemo hiyo ikiwekwa, mikataba sita ya makubaliano kati ya nchi hizo mbili imesainiwa ambapo miongoni mwake inalenga kukuza diplomasia ya kiuchumi na elimu ya juu.
Hayo yamebainishwa katika mkutano wa pamoja kati ya Rais wa nchi hiyo, Recep Tayyip Erdoğan na Rais Samia Suluhu Hassan aliye katika ziara ya siku tano katika nchi hiyo iliyoanza jana Alhamisi Aprili 17, 2024.
Rais Samia anafanya ziara ya kiserikali nchini humo kwa mwaliko wa mwenyeji wake ikiwa ni miaka takribani saba tangu Erdogan alipoitembelea Tanzania Januari 2017.
Akizungumza katika mkutano uliowakutanisha viongozi mbalimbali baada ya marais hao kufanya mazungumzo ya pamoja, Erdogan amesema licha ya kuwa biashara kati ya nchi hizo mbili inazidi kukua lakini bado haijafanyika kiasi cha kutosha.
“Biashara kati ya nchi hizi imeongezeka kutoka Sh28.38 bilioni mwaka 2003 hadi Sh890.1 bilioni mwaka uliopita hatahivyo hicha ya ongezeko hilo lakini bado haliakisi kiwango cha uwezo wetu,” amesema Erdogan.
Amesema makubaliano yaliyowekwa ni kuhakikisha biashara kati ya Tanzania na Uturuki inaongezeka hadi kufikia Sh2.58 trilioni katika siku za usoni.
Katika kufanikisha hilo, Erdogan amesema katika mazungumzo waliyofanya, mbali na kujadili juu ya uhusiano wa nchi hizo mbili pia wameangazia ni hatua gani zinazoweza kuchukuliwa ili kukuza biashara kwa pamoja.
Amesema Tanzania moja kati ya wabia muhimu wa nchi hiyo katika nchi za Afrika ya Mashariki huku akieleza kuwa uhusiano huo wa muda mrefu umekuwa wa heshima na unaomnufisha kila mmoja.
Amesema Tanzania ni nchi ya kwanza katika Bara la Afrika na ya tatu katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambayo miradi mingi inatekelezwa na wakandarasi kutoka Uturuki hasa katika maeneo ya ujenzi ikiwemo reli ya kisasa.
“Ni fahari kwetu kuwa reli ya kisasa inayojengwa Tanzania itakayounganisha takribani nchi nzima inajengwa na kampuni ya uturuki,” amesema Erdogan.
Erdogan amesema Bara la Afrika lina sehemu ndani ya moyo wake huku akieleza kuwa ameshalitembelea zaidi ya mara 50 wakati akiwa ameshika nyadhifa mbalimbali hadi sasa alipokuwa Rais.
“Malengo yetu ni kuimarisha mahusiano yetu na Bara la Afrika katika sehemu nyingi kutoka katika biashara hadi elimu, kilimo na afya,” amesema Erdogan.
Kwa upande wake, Rais Samia ambaye leo ni siku yake ya pili katika ziara hiyo ya kiserikali amesema kesho Ijumaa Aprili 19, 2024 wanatarajia kufanya mkutano wa biashara ambao utawakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Uturuki.
Amesema katika mkutano huo, Tanzania itakwenda kusimamia mambo matatu ambayo ni kuziita Tanzania kutoka Uturuki kuja kuwekeza nchini, kueleza mazingira mazuri na wezeshi ya biashara yaliyopo na namna wafanyabiashara na wawekezaji wanavyonufaika na kile walichokifanya nchini.
“Kuziita kampuni nyingi za biashara na uwekezaji kuja Tanzania kuwekeza katika maeneo ya kimkakati kama usafirishaji, uchumi wa bluu, viwanda, kilimo na utalii,” amesema Samia.
Samia amesema katika majadiliano na Rais Erdogan pia wameangalia namna wanavyoweza kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi hasa katika sekta zenye uzalishaji na kijamii ili kusaidia ukuai wa uchumi.
Samia amesema katika mazungumzo yake na Rais wa nchi hiyo pia amemueleza ni kwa namna gani wataalamu kutoka nchini Uturuki wanavyoisaidia Tanzania katika utekelezaji wa miradi hususani ile ya kipaumbele ikiwemo reli ya kisasa (SGR) ambayo itaiunganisha Tanzania nan chi jirani.
Source: mwananchi.co.tz