Dar es Salaam. Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle ametoa tahadhali ya ongezeko la idadi ya watu nchini akisema linaweza kuwa neema au kinyume chake, huku akisisitiza juu ya umuhimu wa teknolojia ya dijitali ili kulete manufaa zaidi.
Battle amesema hayo leo Alhamisi, Mei 9, 2024 wakati wa mkutano wa wadau wa mawasiliano nchini Tanzania uliokuwa ukijadili matokeo ya utafiti uliozungumzia nguvu ya utaratibu wa minara ya kuchangia katika kukuza sekta ya mawasiliano barani Afrika.
Mwakilishi huyo wa Marekani nchini amesema Tanzania sasa ina watu milioni 61 na kulingana na makadirio ya Shirika la Umoja wa Mataifa, mpaka 2050 idadi hiyo itaongezeka hadi mara mbili yake na karibu watu wote wapo chini ya umri wa miaka 18, hivyo hiyo ni fursa lakini pia changamoto.
“Tukiweza kufanya vizuri kwenye biashara, uwekezaji na maendeleo kwa kutengeneza fursa za ajira kwa vijana na wanawake sanjari na kuwapa elimu ya sayansi kimkakati, hapo ongezeko la watu litakuwa ni mali lakini tukishindwa kufanya hivyo idadi kubwa ya vijana itakuwa ni changamoto,” amesema Battle.
Amesema kundi la vijana likigeuka kuwa changamoto badala ya fursa hata udhibiti wake unakuwa ni mgumu, hususani wasio na ajira wakigeuka kuwa mawindo ya fursa za kigaidi na hatimaye kufanya mambo yasiyo na tija kwa nchi yao.
“Tuna wajibu wa kuhakikisha wingi wa vijana ni mali, faida na fursa hivyo ni muhimu kudhibiti changamoto kabla haijakomaa. Vijana wakipewa elimu nzuri na kuwa na fursa za ajira watakuwa viongozi wa kuleta amani na maendeleo ya nchi na dunia,” amesema Balozi Battle.
Battle amesema miongoni mwa masuala ya kufanikisha hilo ni kuwekeza katika sekta ya mawasiliano ili kuwafanya vijana kuwa wabunifu na kurahisisha mawasiliano yao kibiashara, huku akiweka msisitizo zaidi kwenye matumizi ya akili bandia (AI).
Akiwasilisha matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Telecom Advisory Services, mtafiti Raul Katz amesema minara ya kuchangia imeleta mwenendo mzuri wa usambazaji wa mawasiliano barani Afrika, lakini changamoto iliyobaki sasa ni uwezo wa Waafrika kumudu gharama za mtandao na kusababisha watu wengi kutotumia huduma zilizo karibu yao.
“Gharama ya huduma za mawasiliano katika mataifa mengi ya Afrika zinafikia asilimia 4.4 ya pato lao la mwezi kiwango ambacho ni kikubwa kuliko asilimia mbili inayopendelezwa kimataifa (ITU/UNESCO),” amesema Katz akiwasilisha ripoti ya utafiti huo unaoweka mkazo wa umuhimu wa mawasiliano.
Akizungumzia changamoto zilizopo katika biashara ya minara ya kuchangia, Tudor Samuila amesema mazingira ya uwekezaji Tanzania ni mazuri ikilinganisha na mataifa mengine ambayo kuna hofu ya usalama, hata hivyo amesema changamoto iliyobakia ni suala la umeme ambalo nalo wameweza kulishughulikia kwa kufunga mifumo ya sola.
Akizungumza katika mkutano huo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Serikali inachokifanya sasa ni kupunguza gharama za huduma za simu na kuongeza kipato cha wananchi, ili kuwa na ujumuishi mkubwa katika huduma za kidijitali.
“Kwa kushirikiana na sekta binafsi tunaendelea kupeleka mawasiliano maeneo tofauti nchini na kufanya juhudi za kupunguza gharama za huduma mbali na mapitio ya kikodi, lakini pia tunahamasisha uwekezaji wa minara ya kuchangia ili kupunguza gharama za uendeshaji,” amesema Nnauye.
Ameongoza Serikali inaendelea na utekelezaji wa sera ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano (Tehama) na mpaka sasa imefanikiwa kuongeza usambazaji wa huduma ya mawasiliano, ubora na kasi ya mtandao wa intaneti.
Katika hatua nyingine, Nnauye ametembelea ofisi ya Jamii Forums ambapo alipongeza mpango wao wa kuongeza huduma za mtandao wa intaneti kwa Watanzania wengi wa vijijini, kupitia usambazaji simu janja za bei rahisi wanaotarajia kuufanya siku zinazo.
“Tunajenga mindombinu ya mawasiliano na kwa gharama kubwa, tunavutia wawekezaji na kufanya maboresho lakini utumiaji wa huduma za mtandao bado ziko chini, wananchi wengi wanatumia vitochi hivyo upatikanaji wa simu janja za bei nafuu utaongeza matumizi kwa kiwango kikubwa,” amesema Nnauye.
Naye Mkurugenzi wa Jamii Forums, Maxcence Melo amesema mpango uliopo ni kutengeneza na kusambaza simu janja zaidi ya milioni 10 kwa wakazi wa vijijini na bei yake itakuwa ni dola 20 (Sh50,000) kwa moja na uwezo wake wa kutunza chaji utakuwa hadi siku saba.
Source: mwananchi.co.tz