Askofu mstaafu Dk Mokiwa atoa ushahidi kesi ya ardhi

Askofu mstaafu Dk Mokiwa atoa ushahidi kesi ya ardhi

Askofu mstaafu Dk Mokiwa atoa ushahidi kesi ya ardhi

Dar es Salaam. Aliyekuwa Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa, ameieleza Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, jinsi alivyoshiriki mchakato wa kutoa eneo kwa ajili ya kupewa aliyekuwa Askofu wa kwanza wa dayosisi hiyo na Askofu Mkuu wa kanisa hilo, hayati John Sepeku.

Hayati Sepeku alipewa na kanisa hilo nyumba iliyopo Buguruni na kiwanja chenye ukubwa wa ekari 20 kilichopo Buza wilayani Temeke kama zawadi kwa kutambua mchango wake katika kanisa hilo.

Mokiwa (59) ametoa ushahidi leo Septemba 24, 2024 katika kesi ya ardhi iliyofunguliwa na mtoto wa hayati Sepeku, Bernardo Sepeku dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania na Askofu Jackson Sostenes wa Dayosisi ya Dar es Salaam.

Bernado alifungua kesi ya ardhi namba 378/2023, akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yake mwaka 1978 na kanisa hilo.

Mtoto huyo alifungua kesi dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa Angikana Tanzania, Askofu Jackson Sostenes wa Dayosisi ya Dar es Salaam na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.

Mdaiwa wa tatu katika kesi hiyo, Kampuni ya Xinrong hajawahi kufika mahakamani tangu kesi ilipofunguliwa licha ya kupokea wito wa kuitwa mahakamani hapo.

Bernardo anaomba alipwe Sh3.72 bilioni za fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi katika kiwanja hicho.

Pia, anaomba alipwe fidia ya Sh493.65 milioni ambayo ingepatikana baada ya kukomaa na mavuno ya mazao yaliyokuwepo kwenye ardhi hiyo.

Dk Mokiwa akiongozwa na mawakili Deogratias Butawantemi na Gwamaka Sekela kutoa ushahidi mbele ya Jaji Arafa Msafiri, alianza kumuomba Mungu na kisha kutoa ushahidi uliochukua saa tano.

Dk Mokiwa ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa mlalamikaji, amedai anakumbuka katika rekodi zilizokuwa ofisini kwake kipindi hicho akiwa askofu wa kanisa hilo, za Desemba 8, 1978 kulikuwa na muhtasari wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Kanisa la Anglikana ya jimbo hilo, iliyopendekeza kumpatia mali, Askofu wa kwanza wa dayosisi hiyo na Askofu Mkuu wa kwanza wa kanisa hilo, Sepeku kama zawadi baada ya kustaafu utumishi wake.

“Ukiachana na hiyo, pia nafahamu kuwa baada ya miaka miwili (mwaka 1980), kulikuwa na Sinodi iliyobariki maamuzi yale ya kumpatia John Sepeku ekari 20,” amedai Dk Mokiwa aliyekuwa mwenyekiti wa bodi ya wadhamini wa kanisa hilo.

Sinodi ni mkutano mtakatifu unaojumuisha askofu, mapadri, waumini kwa ajili ya kutoa maamuzi mbalimbali yanayohusu kanisa na maamuzi yanayotolewa katika mkutano huo, hayapingwa sehemu yoyote.

Amedai kikao hicho kilichompa Askofu Sepeku  zawadi kwa kutambua mchango wake katika Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam, kilikuwa ni halali.

“Na kwa utamaduni na sheria, maaskofu wa Kanisa la Anglikana huwa hawatengui maamuzi ya askofu aliyetanguliwa na kama itakuwa hivyo, basi Askofu Jackson Sosthenes wa Dayosisi ya Dar es Salaam atakuwa askofu wa kwanza wa Kanisa la Anglikana Tanzania kutengua maamuzi ya maaskofu wenzake,” amedai Dk Mokiwa.

“Maamuzi ya Sinodi hayawezi kupingwa na askofu yeyote, kwa kuwa yalikuwa ni maamuzi halali,” amedai.

“Kwa kutumia mamlaka yangu, nilimteua mmoja wa wafanyakazi wa kanisa kusimamia mgawanyo, ambazo ni kiwanja namba 13 kilichopo eneo la Kichwere, Buguruni (ambako kuna nyumba) na kiwanja namba 2689 chenye ukubwa wa ekari 20 kilichopo Buza Mtoni,” amedai.

Dk Mokiwa amedai aliheshimu uamuzi wa Sinodi na alifanya sehemu yake kwa kumteua mtu aendelee kushughulikia jambo hilo.

“Nilielekeza watu wangu wafuate utaratibu wa kisheria wa kukamilisha uhamisho wa umiliki,” amedai.

“Mimi kwa sasa ni askofu mstaafu, sijui nini kinaendelea huko, ila hapa nimekuja kutoa ushahidi kuhusu jinsi tulivyompa eneo aliyekuwa askofu wa kwanza wa Kanisa la Anglikana, marehemu John Sepeku,” amedai.

Amedai aliteuliwa kuwa askofu mwaka 2002 hadi 2007 akiwa Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam na kuanzia mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania hadi mwaka 2013.

Baada ya kumaliza ushahidi, wakili wa mdaiwa wa kwanza na wa pili katika kesi hiyo, Dennis Malamba alimuuliza maswali ya dodoso shahidi na hii ni sehemu ya maswali hayo.

Wakili: Wakati ukiwa Askofu Mkuu wa kanisa hilo ulikuwa unatumia katiba ya mwaka gani?

Dk Mokiwa: Katiba ya mwaka 2004.

Wakili: Je katiba ya mwaka 2004 iliondoa uhalali wa maamuzi yaliyofanywa mwaka 1978 kwa kutumia katiba ya mwaka 1970?

Dk Mokiwa: Hapana

Dk Mokiwa: Lakini katiba ya mwaka 2004, haiondoi uhalali wa katiba ya mwaka 1970 na pia maamuzi yaliyofanywa miaka ya nyuma hayaathiriwi na katiba ya mwaka 2004.

Dk Mokiwa: Dayosisi ya Dar es Salaam ilikuwa na bodi kwa katiba ya kwanza ya Dayosisi ya mwaka 1970 na mali zote za Dayosisi hii zilikuwa zinashikiliwa na Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania.

Wakili: Je kikao kilichompa Askofu Sepeku zawadi, kilikuwa na nguvu ya kumpa?

Dk Mokiwa: Ndio kilikuwa na nguvu hiyo na kilikuwa na uhalali wa kutoa zawadi.

Na kwa utamaduni na sheria, maaskofu wa Kanisa la Anglikana huwa hawatengui maamuzi ya askofu aliyetanguliwa na kama itakuwa hivyo, basi Askofu Jackson Sostenes wa Dayosisi ya Dar es Salaam atakuwa wa kwanza wa Kanisa la Anglikana Tanzania kutengua maamuzi ya maaskofu wenzake.

Dk Mokiwa baada ya kuhojiwa na upande wa wajibu madai, wakili Butawantemi aliomba Mahakama ipokee maelezo ya shahidi, kama sehemu ya ushahidi.

Pia, aliomba Mahakama ipokee vielelezo vitatu ambavyo ni muhtasari wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Kanisa la Anglikana kilichoketi Desemba 8, 1978, Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam ya mwaka 1980 na Katiba ya Angikana ya mwaka 1970.

Wakili Malamba alipinga vielelezo hiyo kupokewa mahakamani akidai nyaraka hizo siyo halisi bali ni nakala.

Amedai anapinga nyaraka hizo zisipokewe kwa kuwa hawakupewa notisi za kuleta vielelezo halisi mahakamani hapo.

Butawantemi amedai walishawasilisha notisi hiyo mahakamani hapo na kama takwa la kisheria ya ushahidi linavyoeleza.

Baada ya Mahakama kujiridhisha na nyaraka hizo, ilitupilia mbali pingamizi la wakili Malamba na kupokea vielelezo hivyo.

Jaji Msafiri ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 30 na Oktoba 31, 2024 itakapoendelea kwa shahidi wa pili wa upande wa mlalamikaji kutoa ushahidi.

Awali, kabla ya Dk Mokiwa kutoa ushahidi, Mahakama ilitupilia mbali pingamizi lililowekwa na wadaiwa katika kesi hiyo la kutaka mashahidi watano kati ya 10 akiwamo Dk Mokiwa wasitoe ushahidi kutokana na viapo vyao kuwa na kasoro za kisheria.

Akitoa uamuzi, Jaji Msafiri amesema mapingamizi yaliyowekwa hayana mashiko kwa kuwa yaliwasilishwa kabla ya muda wa kutolewa kwa ushahidi.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories