Mbeya. Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa amesema Wakristo wengi hivi sasa wamesahau thamani yao na kuanza kujifananisha na kila mtu.
Dk Malasusa ameyasema hayo leo Jumapili Julai 7, 2024 wakati wa kuweka wakfu Kanisa la KKKT Dayosisi ya Konde Usharika wa Foresti Mpya jijini Mbeya, ambalo ujenzi wake umegharimu zaidi ya Sh1.2 bilioni.
Amesema; “Mara nyingi Wakristo tumesahau juu ya thamani tuliyonayo, tunadhani tunafanana na kila mtu. Sisi tumetengwa kwa kazi maalumu. Huwa nasikitika sana kuulizwa huyu anajishughulisha na nini akajibu ‘niponipo tu’.”
Amesema lazima wajitofautishe hata kwa kufanya kazi na biashara pia.
Askofu huyo amesema kama waumini wa Kikristo pia watasimama kupinga rushwa ambayo ni tatizo kubwa nchini, huenda nayo isingekuwepo.
Dk Malasusa amesema Wakristo wamekuja kwa kazi maalumu, hivyo lazima wajithamini na kuwa tofauti kwa kufanya shughuli yoyote, hata kuuza mchicha, ili kulinda thamani yao.
Amesema lazima kila mmoja ajifanyie tathmini juu ya maisha yake na kusimama imara kanisani kupinga vita ya kutoa na kupokea rushwa ili kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano hayo.
Amelitaka pia kanisa hilo kuanzia ngazi ya Usharika, Jimbo hadi Taifa kuhubiri umoja, mshikamano na upendo huku akisisitiza kwamba Mungu anahitaji umoja ndani na nje. Ameongeza kuwa njia sahihi ya kuondoa na kukabiliana na uadui ni kulishika neno la Mungu, akieleza kuwa Mkristo lazima awe nuru katika giza kwa kumuamini Mungu.
“Tunatamani kuona kanisa hili la Foresti likifika mbali. Leo tunaweka wakfu jengo hili la thamani. Kanisa ni sisi wenyewe kwa matendo yetu, hivyo tujitolee kwa ajili ya Mungu,” amesema Askofu Malasusa.
Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mbeya, Patrick Mwalunenge akizungumza katika hafla hiyo amewataka waamini na viongozi wa dini kuhubiri upendo na kusameheana, akieleza kuwa wote ni binadamu. “Tuache kuwekeana visasi, tutumie majukwaa yetu kuhubiri amani, upendo na mshikamano, lakini kusameheana kwa kuwa sote ni binadamu na tunayo mapungufu,” amesema Mwalunenge.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amesema kupitia kanisa, wanaamini kitazalishwa kizazi cha maadili na Taifa jasiri, huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za dini kujenga miradi ya maendeleo kwa wananchi.
“Kwa niaba ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, anachangia Sh1 milioni na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Sh500,000, lakini tunaahidi kuwa pamoja na ninyi muda wowote,” amesema Malisa.
Naye mmoja wa wachungaji, Elisha Enos amesema tukio hilo limekuwa na tija katika kujenga kanisa kubwa ikiwa ni baraka na utukufu kwa Mungu katika kueneza injili.
“Hili ni agizo la Mungu katika kuwa na umoja, hivyo usharika huu, jimbo na Dayosisi hii ya Konde lazima tuendelee kujenga umoja na kumtukuza Mungu kwa njia ya umoja,” amesema mchungaji huyo.
Source: mwananchi.co.tz