Sumbawanga. Aliyefungua kesi ya kudai fidia ya zaidi ya Sh306.6 akwaa kisiki Mahakama Kuu Tanzania.
Limi Mchome mwenye ualbino, alifungua kesi ya madai akiwadai Kamanda wa Polisi (RPC) Mkoa wa Katavi na wenzake wawili, zaidi ya Sh306.6 milioni kama fidia, baada ya watu wasiojulikana kuukata mkono wake wa kulia na kuondoka nao, licha ya kuwahi kutoa taarifa ya uwepo wa watu waliokuwa wakimfuatilia.
Uamuzi wa kuitupa kesi hiyo ulitolewa jana Jumatatu, Agosti 26, 2024 na Jaji Abubakar Mrisha wa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga, na kumwamuru pia alipe gharama za kesi baada ya kukubaliana na pingamizi la awali lililowasilishwa na wadaiwa.
Limi alikatwa mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana na wakaondoka nao, hivyo akafungua kesi ya madai akidai fidia hiyo kwa kile alichodai ni uzembe wa RPC na wenzake kutochukua hatua ya kuzuia uhalifu huo.
Katika madai yake alisema miezi kadhaa kabla ya kukatwa mkono, mkuu wa upelelezi Mkoa (RCO) Katavi, alijulishwa juu ya uwepo wa kundi lililokuwa likimtafuta, lakini hakuchukua hatua ya kumlinda, wakati huo akiwa na umri wa miaka 30.
Tukio hilo lilitokea usiku wa Julai 14, 2015 katika Kijiji cha Mwachona Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, watu wasioujulikana walivunja mlango wa chumba alichokuwa amelala, huku wakimfungia kaka yake kwa nje ili asitoke.
Limi alifungua kesi ya madai namba 6 ya 2023 dhidi ya RPC Katavi kama mdaiwa wa kwanza, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kama mdaiwa wa pili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama mdaiwa wa tatu.
Hata hivyo, wadaiwa hao waliwasilisha pingamizi la awali wakisema kesi hiyo ni mbaya mbele ya macho ya sheria kwa kuwa imefunguliwa nje ya muda wa miaka mitatu unaoruhusiwa kisheria, hivyo wakaiomba mahakama iitupilie mbali kesi hiyo.
Katika kesi hiyo, Limi anayejulikana pia kama Remi Luchoma, aliomba alipwe Sh215 milioni kama fidia ya kukatwa mkono wake wa kulia na Sh85 milioni kama kipato ambacho angepata kama angekuwa na mkono wake kwa miaka 35.
Mbali na madai hayo, alikuwa anadai Sh5 milioni kama malipo ya kupoteza huduma, apewe matunzo ya watoto wake ikiwamo kuwasomesha kwa kuwa hana tena uwezo wa kuwasomesha lakini pia kupatiwa mkono wa kisasa wa bandia.
Hoja za kisheria za pingamizi
Baada ya kufungua kesi hiyo, wadaiwa wakiwakilishwa kortini na wakili wa Serikali Mjahidi Kamugisha, waliwasilisha pingamizi la awali wakisema kesi hiyo imepitwa na muda (time barred) huku Limi akiwakilishwa na wakili Gadiel Sindamenya.
Akitetea pingamizi la awali, wakili Kamugisha alisema kwa kuangalia hati ya madai, kiini chake ni madai ya uzembe na kwamba madai ya aina hiyo yanatakiwa yafunguliwa mahakamani ndani ya muda wa miaka mitatu tangu uzembe utokee.
“Hii ina maana muda wa kikomo wa kufungua shauri hilo kwa uzembe uliotokea Julai 13,2013 ulimalizika Julai 14,2015. Huu ndio msimamo wa sheria. Madhara ya kufungua kesi nje ya muda ni mahakama kuitupa kwa gharama,” alisema.
Hata hivyo, wakili Sindamenya aliyekuwa akimtetea Limi katika hoja zake alisema pingamizi hilo halina mashiko akisema hoja za wadaiwa zimejikita katika kipengele cha 6 cha sheria ya ukomo sura ya 89 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019.
Kwa maoni yake alisema hiyo sio sawa na ni madai yenye makosa makubwa na kueleza kuwa kosa hilo lilitendeka Julai 14, 2015, upelelezi ukafanyika na watu sita wakakamatwa na kufikishwa kortini kwa kosa la kujaribu kumuua Limi.
Wakili huyo aliongeza kusema kuwa Oktoba 23,2019, washitakiwa 5 walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela, akieleza ilikuwa vigumu kufungua kesi kwa wadaiwa wakati kesi ya jinai ilikuwa bado inaendelea kortini.
Alieleza kuwa baada ya washitakiwa kutiwa hatiani, Limi alikusanya ushahidi wa uzembe anaoulalamikia wa Mkuu wa Upelelezi mkoa (RCO) Mkoa wa Katavi kwa kushindwa kutimiza wajibu wake wa kulinda raia na mali zao.
Zaidi ya hayo, Sindamenya alisema kulikuwa na siku 60 za kukata rufaa baada ya hukumu ambazo zilimalizika Desemba 23, 2019 na kwamba ni kanuni ya asili kuwa hukumu ya Mahakama Kuu ni lazima ipate baraka za Mahakama ya Rufani.
Wakili huyo alieleza kuwa Februari 8, 2021 alitoa notisi ya siku 90 kwa wadaiwa, hivyo kwa kuhesabu kuanzia siku ya hukumu hadi siku ambayo alifungua kesi hiyo ya madai, kesi hiyo itakuwa ilifunguliwa ndani ya muda wa kisheria unaotakiwa.
Aliiomba mahakama kuzingatia ibara ya 107(A)(2)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuepuka kufungwa na mambo ya kiufundi ambayo yananyima haki ya msingi, hivyo alitupe pingamizi hilo na kusikiliza kesi ya msingi.
Uamuzi wa jaji ulivyokuwa
Akisoma uamuzi wake kuhusiana na pingamizi hilo, Jaji Mrisha alisema ni jambo ambalo halibishaniwi kuwa mdai alifungua kesi hiyo ya madai ya uzembe dhidi ya wadaiwa, lakini hoja iliyoko mbele yake ni kama kesi imefunguliwa nje ya muda.
Jaji Mrisha alisema mawakili wa pande mbili wanakubaliana kuwa msingi wa kesi hiyo ni madai ya fidia, yanayotokana na uzembe na muda wa kisheria wa kufungua kesi ni ndani ya miaka mitatu na kwamba huo ndio msimamo wa sheria.
Alisema madai ya mdai ni uzembe uliosababishwa na wajibu maombi kwa kushindwa kumlinda asikatwe mkono na kueleza kuwa msingi wa uzembe huo ulitokea 14 Julai 2015, lakini kesi ilifunguliwa Julai 17, 2023.
“Hii inaonyesha ni baada ya miaka sita. Kwa hiyo mdai (Limi) alipaswa kufungua kesi ya madai ya uzembe uliotokea ndani ya miaka mitatu,” alisema Jaji Mrisha.
Hata hivyo, Jaji Mrisha alisema katika wasilisho la mdai aliondoa muda wa usikilizwaji wa kesi ya jinai na tarehe ya hukumu na akaondoa pia muda wa washitakiwa kukata rufaa pamoja na siku 90 za notisi aliyowapa wadaiwa.
Alisema ni msimamo wa sheria kuwa pale kesi inafunguliwa baada ya kupita muda uliowekwa na sheria, mdai ni lazima aonyeshe kwenye hati ya madai sababu za upekee wa kesi yake na Jaji akarejea baadhi ya kesi zilizobeba msimamo huo.
Kutokana na msimamo huo, Jaji alisema alipata muda wa kupitia hati ya madai ya kesi hiyo iliyofunguliwa Julai 17, 2023 na kugundua hakuna aya ambayo mdai anaelezea sababu za kupata msamaha wa kutozingatia sheria ya ukomo.
“Hata kama nitachukua wasilisho lake kuwa mdai alichelewa kufungua kesi kwa sababu alikuwa akisubiri ushahidi wa kutosha katika kesi ya jinai iliyokuwa ikiendelea kortini, kwa maoni yangu sababu haina mashiko mahakama kuikubali,” alisema.
Jaji akaongeza kusema “Msimamo wa sheria uko wazi kwamba mwathirika katika kesi ya jinai hazuiwi kufungua shauri la madai ya fidia mahakamani, kwa kuwa mahakama ya jinai sio sahihi kupima madai ya mtu anayeomba fidia”
Katika uamuzi wake huo, Jaji Mrisha alisema suala la ukomo wa muda ni jambo linalokwenda kwenye mzizi wa mamlaka ya mahakama na haiangukii katika Ibara ya 107(2)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Jaji alisema kwa hoja alizozieleza anakubali pingamizi lililowasilishwa na wadaiwa na kukubaliana nao kuwa kesi imefunguliwa nje ya muda, hivyo inatupiliwa mbali na mdai atawajibika kulipa gharama za kesi hiyo.
Source: mwananchi.co.tz