ACT-Wazalendo wapinga uchaguzi Zanzibar kufanyika siku mbili

ACT-Wazalendo wapinga uchaguzi Zanzibar kufanyika siku mbili

Unguja. Chama cha ACT-Wazalendo kimesisitiza msimamo wake wa kupinga uchaguzi mkuu kufanyika siku mbili visiwani Zanzibar, kikitaka ufanywe siku moja.

Mwenyekiti wa chama hicho, Othman Masoud Othman amesema hawatakubali jambo hilo liendelee.

Othman ambaye pia ni makamu wa kwanza wa Rais visiwani humo, anakuja na hoja hiyo ilhali ni takwa la kisheria iliyotungwa kwa lengo la kutoa fursa kwa makundi mbalimbali kupiga kura.

Mara kadhaa uchaguzi wa Zanzibar siku ya kwanza, hutumiwa na watumishi wa umma wenye kazi maalumu, zikiwamo za vyombo vya ulinzi na usalama na siku pili ndiyo kwa wananchi wote.

Mtindo huo wa upigaji kura umekuwa ukipingwa na baadhi ya vyama vya upinzani.

Othman ameeleza hayo jana katika mkutano wa hadhara wilayani Wete, Mkoa wa Kaskazini ukiwa ni miongoni mwa mikutano waliyoipa jina la ‘Bandika bandua’ inayofanyika kwa siku nne Pemba.

Amesema chama hicho kilishaomba kuondolewa utaratibu wa uchaguzi kufanyika kwa siku mbili, lakini Serikali haijajibu.

“Kama watu wanajiamini wanatakiwa wazingatie Katiba, waingie uwanjani, masanduku ya kura ndiyo yaamue mwenye nguvu,” amesema.

Othman amesema jambo hilo linairudisha nyuma Zanzibar na iwapo Serikali haitatekeleza matakwa yao, hata uchaguzi wa siku moja pengine usifanyike.

“Ndugu zangu nawaambia nyuso zetu zinaonyesha tumechoka, haya yanaturudisha nyuma kila siku hatuendi mbele, tunachowaambia hatuwezi kukubali haya viongozi wenu, hatutofanya uchaguzi si tu wa siku mbili, hata wa siku moja na robo hautafanyika,” amesema Othman.

Wakati huohuo, amesema Zanzibar ina uwezo kupata maendeleo zaidi ya mataifa mengi, lakini kukosekana kwa viongozi waadilifu ndiko kunakokwamisha suala hilo.

Othman aliirejea bajeti ya Serikali akisema makusanyo ni Sh1.5 trilioni, kati ya hizo Sh900 bilioni zinalipa mshahara na Sh300 bilioni zinalipa madeni, hakuna fedha zinazobaki kwa ajili ya maendeleo.

Kwa sababu hiyo, amesema visiwa hivyo vitabaki kuwa maskini kama mfumo hautabadilishwa.

Othman ametaja jambo lingine linalokwamisha maendeleo visiwani humo ni kukosekana mamlaka ya kujiamulia mambo yake yenyewe na vitu vingi vimeingizwa katika masuala ya Muungano akitaja zaidi ya 41.

Baadhi ya mambo hayo ni ushuru wa forodha, gesi na mafuta, sarafu, ushuru wa bidhaa, bandari, elimu ya juu, usafiri wa anga, takwimu, leseni za viwanda na bandari.

“Mambo 41 yote yapo kwenye Muungano, wewe unasema una Serikali na kujikweza nipo kwenye chama tawala, unatawalaje? Wengine wanasema maneno lakini hawajui hata wanayosema, leo ukiambiwa hauna mamlaka katika mambo hayo maana yake hauna mamlaka katika kuendesha uchumi wa nchi yako,” amesema Othman.

Amesema wanaposema wanapambania mamlaka kamili ni kwa sababu wanajua uhalisia wa mambo na wakipata mamlaka hayo watajikwamua kutoka kwenye umaskini.

Awali, makamu mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Ismail Jussa amesema Pemba ndiyo mwalimu wa siasa visiwani humo, hivyo wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika vuguvugu hilo la mabadiliko.

Amesema baada ya Uchaguzi Mkuu 2020, Maalim Seif Sharif Hamad alizunguka kutafuta maoni kwa wananchi na wakakubaliana kuingia katika SUK (Serikali ya Umoja wa Kitaifa) kwa masharti ambayo yameshindwa kutekelezeka.

Amesema Maalim Seif (aliyefariki dunia Februari 17, 2021) alikuwa akisisitiza umoja, mshikamano na utekelezaji wa makubaliano, lakini alifariki dunia bila hayo kufanikiwa.

Hata hivyo, amesema licha ya Maalim Seif kufariki dunia, chama hicho hakijapoteza kwa kuwa kimempata mrithi sahihi wa nafasi yake.

“Maalim kaondoka sasa tumempeleka Othman, ili mwaka 2025 akawafundishe namna Serikali inavyoongozwa,” amesema.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Source: mwananchi.co.tz

Original Media Source

Share this news

Facebook
Twitter
LinkedIn
WhatsApp

This Year's Most Read News Stories

Popular
Swahili News Editor

MGAO WA MAJI WAWATESA WAZANZIBARI

Wananchi wengi hasa katika maeneo ya Mjini Unguja, wanalalamikia ukosefu wa maji safi na salama huku Mamlaka ya Maji Zanzibar ikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ujuzi na wataalam katika masuala ya uandisi wa Maji na fani nyengine.Continue Reading

Muslims in Pemba conduct special prayer against ZAA decision
Popular
Investment News Editor

Muslims in Pemba conduct special prayer against ZAA decision

ZANZIBAR: More than 200 Muslims in Vitongoji Village, South Pemba Region over the weekend conducted a special prayer to condemn the Zanzibar Airports Authority (ZAA) move to appoint DNATA as the sole ground handler in Terminal III of the International Airport of Zanzibar. Abeid Amani Karume.Continue Reading